Mmiliki wa Shule ya Sekondary ya St. Patrick ya jijini Dar es Salaam, Ndele Mwaselela amejitolea kumsomesha mtoto wa marehemu Agnes Masogange, Sania(11) kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na akifaulu hadi chuo kikuu.
Hii ni neema nyingine kwa mtoto huyo wa pekee wa Masogange aliyemuacha, baada ya jana kamati ya maandalizi ya mazishi kupitia mweka hazina wake, Zamaradi Mketema kueleza kuwa wamemwekea Sh2 milioni zilizobaki katika michango ya msiba huo kwenye akaunti yake.
Zamaradi amesema fedha hizo zimewekwa mahususi kwa ajili ya kumsaidia kianzio katika cha ada atakapoanza kidato cha kwanza mwakani kwa kuwa mwaka huu anatarajiwa kumaliza darasa la saba.
Akizungumza Leo Jumatatu Aprili, 23, 2018 katika shughuli za mazishi, zilizofanyika nyumbani kwa baba wa Masogange, Kijiji cha Utengule, Wilaya ya Mbalizi, Mwalesela amesema mbali ya kumsomesha pia mtoto huyo atakaa hosteli kwa gharama zake kwa muda wote wa masomo yake.
“Akifaulu kidato cha nne pia atasomeshwa na mimi hadi kidato cha tano na sita lakini pia akifaulu atakwenda hadi chuo kikuu,”amesema Mwaselela.
Kutokana na maamuzi hayo, alimtaka msanii Irene Uwoya ambaye mtoto wake naye anasoma katika shule hiyo, kuhakikisha anapokwenda kumsalimia mwanaye awe anakwenda kumsalimia na Sania.
“Hivyo wewe msanii Uwoya una mtoto wako pale shuleni kwangu naomba ukija kumuona hakikisha unamuona na mtoto huyo,” amesema Mwaselela.
Pia shughuli za mazishi ya Marehemu Agnes Masogange, zimelazimika kusimama kwa muda baada waombolezaji jijini Mbeya kutaka kupiga picha na wasanii waliofika kijijini Utengule kwa baba yake atakapozikwa.
Agnes Masogange aliyefariki Aprili 20, 2018, akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Mama Ngoma, aliagwa jana Jumapili na mamia ya watu katika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam na baadaye kusafirishwa kuelekea Mbeya.
Katika safari hiyo baadhi ya wasanii wamejumuika na wadau mbalimbali wa masuala ya burudani.
Ujio wao katika msiba huo umekuwa ni neema pia kwa wakazi wa Kijiji cha Utengule na vitongoji vyake, ambao wamekuwa na shauku ya kuwaona wasanii hao macho kwa macho kwani wamekuwa wakiwaona kwenye televisheni na kuwasoma kwenye magazeti na mitandaoni.
Kulunzifikra blog ilishuhudia baadhi ya watu waliowekwa kwa ajili ya kulinda usalama eneo hilo wakiwatuliza watu waliokuwa wakisukumana kutaka kupiga picha na wasanii hadi ratiba kushindwa kuanza kwa wakati kama ilivyopangwa.
Shughuli za kuuaga mwili wa Masogange kijijini hapo zilitarajiwa kuanza saa 6:30 mpaka saa 7:00 na kuzikwa saa 7:30.

No comments:
Post a Comment