Miongozo na taarifa kwa Spika wa Bunge inavyowapotezea muda Wabunge. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 22 April 2018

Miongozo na taarifa kwa Spika wa Bunge inavyowapotezea muda Wabunge.

 
Kuomba utaratibu kwa wabunge ni jambo ambalo limekuwa likiruhusiwa kikanuni, lakini hata hivyo limekuwa likichukua muda mwingi katika baadhi ya mijadala na hivyo kufanya idadi ya wachangiaji kuwa ndogo kuliko ilivyopangwa.

Ingawa taarifa ni muhimu katika uchangiaji kutokana na kulenga kurekebisha kauli ama kumuongezea takwimu mchangiaji, lakini imekuwa ikisababisha kero kwa wanaosikiliza na hata wachangiaji wenyewe.

Kero inasababishwa na kukosekana kwa mtiririko wa hoja ama jambo linalozungumzwa kwa wakati huo na wakati mwingine kutoeleweka kwa kile kinachozungumzwa.

Mifano inaweza kuwa mingi, lakini mkutano wa 11 ambao katika mijadala ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi ya Rais hali hiyo imejidhihirisha kwa wabunge kadhaa kuombewa utaratibu wakati wakichangia.

Hali hiyo licha ya kuleta shida kwa wachangiaji na wasikilizaji, inaonekana kuwa kero pia kwa wenyeviti wa vikao vya bunge kutokana na kushindwa kumaliza orodha iliyopangwa kwa ajili ya kuchangia siku husika.

Mmoja wa wenyeviti wa Bunge, Mhe Andrew Chenge analazimika katika moja ya kikao chake kusema kwa sababu ya miongozo, majibu yake pamoja na taarifa ndiyo imesababisha kutomalizika kwa orodha ya wachangia kwa siku hiyo.

“Sasa uwiano wetu wa vyama vinavyowakilishwa humu bungeni CCM kwa siku nzima tunaweza kuchangia wabunge 32 tu. Sasa kwa uwiano wa wakilishi wa vyama vinavyowakilishwa humu bungeni mnajua tunavyofanya, sita Chadema wanne CUF,” alisema Mhe Chenge.

Hata hivyo, muda wa kuchangia kwa mawaziri wanapowasilisha hoja hupewa dakika 30 na wabunge wakati wa kuchangia hutumia dakika 10 na wakati wa kujibu hoja mawaziri hupewa dakika 10.

Mfano wa taarifa

Mfano wa taarifa kwa wanaochangia mjadala, ni wakati mbunge wa Viti Maalum (CCM), Martha Mlata alipokuwa akichangia mjadala huo unauhusisha Ofisi za Rais ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, alikuwa akikatizwa na taarifa zilizokuwa zikitolewa na wabunge wenzake.

Mbunge huyo katika mchango wake aliomba kupelekewa salamu Rais John Magufuli awasaidie katika kupata upinzani utakaowaletea maendeleo nchini.

Mlata wakati akiendelea kuchangia, ghafla aliibuka mbunge wa Rombo (Chadema)  Mhe Joseph Selasini akitaka kumpa taarifa mchangiaji kwamba Tanzania ina upinzani imara na ndio maana CCM ikawakataza kwenda kwa wananchi kueleza sera zao kwa sababu ya hofu.

Hata hivyo, Mlata alisema taarifa hiyo anaikataa kwa sababu hakuna upinzani ambao unaenda kuwahadaa wananchi wasifanye kazi za maendeleo.

Wakati Mlata akiendelea kuchangia, aliibuka mbunge wa Tanga Mjini (CUF),Mhe  Mussa Mbarouk ambaye alisema wao ni vyama vya mageuzi na si upinzani.

“Upinzani ni huyu anajenga nyumba na huyu anavunja. Sisi ni kioo cha Serikali usitusababishie, tukasema mambo mengine huku hali ichafuke,” alisema Mhe  Mbarouk.

Lakini, wakati Mlata akiendelea kuchangia, aliibuka mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo),  Mhe Zitto Kabwe ambaye aliomba taarifa akitumia kanuni ya 64 kumtaka mchangiaji ajielekeze kwenye hoja na si nje ya mjadala.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge,Mhe  Azzan Zungu akijibu taarifa hiyo alisema hakuna kanuni yoyote iliyovunjwa na Mlata na kumtaka asibweteke na kutoka kwenye hoja.

Wakati Mlata akiendelea kuliibuka wabunge wengine ambao walikuwa wakiomba kutoa taarifa ila walikataliwa na  Mhe Zungu.

Muda mchache wa kuchangua

Hata hivyo, Mhe Zungu alisema inakuwa shida katika shughuli za uendeshaji wa Bunge, lakini kwa sababu ni haki yao lakini ukweli ni kwamba baadhi ya taarifa (akimaanisha zile zisizo muhimu) zinawalia muda.

Kumekuwa na malalamiko ya muda kutotosha kwa baadhi ya wachangiaji bungeni katika bajeti zinazowasilisha, hasa kutokana na wizara nyingi kupangiwa siku moja ama mbili ya kufanya mjadala na kuhitimisha.

Miongoni mwa wabunge wanaona shida ya muda uliopangwa wa kuchangia ambao licha ya kuwa mdogo unaliwa na taarifa na miongozo ni mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Mhe Pauline Gekul.

Mhe Gekul alisema hawapati nafasi ya kuhoji mafungu wakati Bunge linavyokaa kama kamati kupitisha mafungu ya bajeti, na kwamba hafahamu kama hilo linalotokana na upangaji wao wa ratiba za bunge.

Mhe Gekul Alisema kuwa Bunge linavyokaa kama kamati ya bunge zima, wanaruhusiwa kushika shilingi kwenye mshahara wa waziri tu na katika vifungu vingine wananyimwa.

“Katika vifungu vingine mtu hawezi kutoa shilingi kwa kutoa ufafanuzi kwa madai kuwa muda ni mdogo,” alisema  Mhe Gekul.

Baadhi ya wabunge wanaliona tatizo la muda kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na maombi ya utaratibu pamoja na miongozo, linapoteza muda uliopangwa na bunge kuchangia hoja mahususi iliyopangwa kwenye siku husika.

Mbunge wa Rufiji (CCM),  Mhe Mohamed Mchengerwa alisema baadhi ya utaratibu na miongozo inayoombwa inatokana na wabunge wengi kutosoma kanuni za Bunge, kuzijua na kuzitumia ipasavyo mahali zinapotakiwa.

“Kuna mambo ambayo hupaswi kuongea bungeni, hoja ambayo haihusiki kwa wakati huo. Haya mambo yametolewa ufafanuzi katika kanuni zetu,” alisema Mhe Mchengerwa.

Mhe Mchengerwa alisema lakini mbunge anatakiwa kusoma kanuni kuelewa ni lugha inayofaa kutumiwa , wakati wa kuchangia au kuuliza swali.

Pia Mhe Mchengerwa alisema vitendo vya kuomba utaratibu wakati mbunge mwingine akiwa anachangia vina madhara, ikiwamo kumpoteza mzungumzaji katika mtiririko wake wa uchangiaji.

“Hii inaweza kumtoa kwenye ‘reli’ mbunge anayechangia na wengine hufanya hivyo kwa nia ya kuwatoa wabunge katika reli,” alisema Mhe  Mchengerwa ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria.

Aidha,Mhe Mchengerwa alisema pia muda wa wabunge kuchangia katika hoja husika unakuwa mdogo kwa sababu unaliwa na waomba utaratibu na miongozo.

“Kuna baadhi wanataka kuwavuruga wachangiaji. Lengo lao ni kuwaondoa wachangiaji katika reli (mtiririko). Ukimkatiza mtu kuzungumza ni wengi wanashindwa kurudi katika hoja wanaporuhusiwa kuendelea kuchangia kwenye mjadala,” alisema Mhe Mchengerwa.

Hata hivyo, Mhe Mchengerwa alisema uvumilivu unatakiwa wakati mbunge anapochangia kwa kuwasikiliza hadi wanapomaliza hata kama kuna mbunge ambaye hapendi kusikia kinachozungumzwa.

“Wabunge ni wawakilishi wa wananchi na wanachokiongea wanakuwa wametumwa na wapiga kura wao, hata kama hutaki kusikia jambo hilo uwe mvumilivu amalize kuchangia,” alisema Mhe Mchengerwa.

Mhe Mchengerwa anasema ni vyema wakakubali kuwa hata kama wao hawataki kusikia kile wanachosema wabunge wenzao, kuna wengine ambao wanataka kusikia.

Mhe Mchengerwa alisema ni vyema wakapata fursa ya kupitia upya kanuni zao na kurekebisha, ili kutotoa nafasi kwa wabunge wanaotaka kutumia mwanya huo kuwavuruga wachangiaji.

Mbunge wa Konde (CUF), Mhe Khatib Said Haji anasema wanaoomba kuhusu utaratibu wengi wao hawapendi kusikia kile kinachosemwa na mbunge anayechangia kwa wakati huo, hata kama ni ukweli unaozungumzwa.

“Unajua wengine hawaupendi ukweli na kwa hiyo ili kumtoa katika reli (mtiririko) mzungumzaji basi wanaomba mwongozo ama utaratibu na hii inakuaga ngumu sana kwa wabunge wapya kurejea tena katika mstari baada ya kuruhusiwa kuongea,” alisema Mhe Haji.

Hata hivyo, Mhe Haji alisema wabunge wazoefu, utaratibu umekuwa sio shida kwao kwa sababu wanafahamu jinsi ya kuukabili na kuendelea kusimamia hoja zao bila kuvurugwa.

“Lakini, kwa wabunge wazoefu wanajua namna ya kuepuka kutoka katika reli na wakiombewa taarifa wanarudi palepale walipokuwepo,” alisema Mhe Haji.

Mhe Haji alisema kuwa ni vyema wabunge wakaachiwa kuongea hadi watakapomaliza, hasa kama hatendi kosa la jinai kwa sababu mbunge ni mwakilishi wa watu bungeni.

Hata hivyo, Mhe Haji alisema miongozo na taarifa inategemea kiti kinachoongoza bungeni wakati huo kwa sababu wana uwezo wa kutambua lengo la mbunge husika.

“Kiti (mwenyekiti ama spika) kina uwezo wa kujua taarifa hii inayotolewa sasa sio muhimu kutokana na mwenendo wa mchangiaji,” alisema Mhe Haji.

No comments:

Post a Comment

Popular