Jeshi la polisi linamshikilia Mbunge wa Chadema pamoja wafuasi 27 wa Chadema. - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 3 April 2018

Jeshi la polisi linamshikilia Mbunge wa Chadema pamoja wafuasi 27 wa Chadema.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linamshikilia Mbunge wa Tarime Vijini, Mhe John Heche (Chadema), kwa tuhuma za kushindwa kuripoti polisi kama alivyotakiwa Jeshi hilo.

Akizungumza na kulunzifikra blog, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amethibitishwa kushikiliwa kwa mbunge huyo.

Mambosasa amesema Mhe  Heche alikamatwa kwa kosa sawa na lile lililokuwa likimkabili Mbunge wa Kawe, Mhe  Halima Mdee, ambaye pia alishindwa kuripoti polisi wiki iliyopita baada ya kwenda Afrika Kusini kwa matibabu kabla ya kukamatwa Uwanja wa Ndega wa Dar es Salaam (JNIA), usiku wa kuamkia juzi.

Aidha, kamanda Mambosasa amesema endapo taratibu zitakamilika mbunge huyo anaweza kufikishwa mahakamani kesho, kuunganishwa katika kesi ya viongozi wengine wa chama hicho waliopata dhamana leo.

“Ni kama alivyoshikiliwa mwenzake Mdee naye hakuripoti, walikuja wakatakiwa kurudi wote wao hawakurudi, hakuna kosa jipya kosa lake ni kutorudi hadi wenzake wanapelekwa mahakamani,” amesema kamanda Mambosasa.

Machi 27 mwaka huu Mhe  Heche alishindwa kuripoti polisi pamoja na viongozi wengine saba wa chama hicho kama walivyotakiwa na jeshi hilo akidai alikuwa na msiba.

Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Chadema, Mhe  Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho, Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, Mhe John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Tarime Mjini, Mhe Esther Matiko ambao wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwamo kuhamasisha maandamano, uchochezi na uasi.

Pia Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia watu 27 wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema kwa tuhuma za kufanya fujo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ikiendelea mahakamani hapo.

Kwa mujibu wa Kamanda Mambosasa wanaoshikiliwa ni wanaume 20 na wanawake saba, ambao walikamatwa katika eneo la Mahakama hiyo wakifanya fujo wakati wakisubiri uamuzi wa Mahakama hiyo juu ya hatima ya dhamana viongozi hao saba wa Chadema.

“Watu hao walikuwa wanafanya vurugu katika eneo la Mahakama wakati Mahakama inaendelea, tumewashikilia na tutawafikisha mahakamani tukikamilisha taratibu,” alisema kamanda Mambosasa.

No comments:

Post a Comment

Popular