Ester Bulaya afikishwa mahakamani. - KULUNZI FIKRA

Monday, 16 April 2018

Ester Bulaya afikishwa mahakamani.

Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Mhe  Ester Bulaya amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuripoti kituo kikuu cha polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Mhe Bulaya amepelekwa Kisutu Leo Jumatatu Aprili 16, 2018 ambako ameungana na viongozi wengine wa chama hicho wanaosubiri kesi dhidi yao kutajwa.

Hivi karibuni mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe John Heche alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka matatu na kuachiwa kwa dhamana.

Mhe Heche aliunganishwa na viongozi wengine wa chama hicho wanaokabiliwa na mashtaka ya kuchochea chuki wanayodaiwa kuyatenda Februari 16, 2018 katika maeneo ya viwanja vya Buibui na Barabara ya Kawawa wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Viongozi wengine wa Chadema ambao wamesharipoti mahakamani ni naibu katibu mkuu (Bara), Mhe John Mnyika; mwenyekiti wa Bawacha,Mhe  Halima Mdee; mwenyekiti Kanda ya Serengeti, Mhe John Heche; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; katibu mkuu wa Chadema, Dkt  Vincent Mashinji; na mweka hazina wa Bawacha, Esther Matiko.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ambao wamefika mahakamani ni mwenyekiti wa Chadema, Mhe Freeman Mbowe na naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa walifikishwa mahakamani Machi 27, 2018.

No comments:

Post a Comment

Popular