Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupandishwa kizimbani. - KULUNZI FIKRA

Friday, 9 March 2018

Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupandishwa kizimbani.

 
Mahakama Kuu ya Tanzania imemuamuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kuwasilisha majibu yake kuhusu kesi za Kikatiba zilizofunguliwa na wananchi 28 ikiwemo kupinga Jeshi la Polisi kuzuia maandamano.

Akizungumza na waandishi wa habari, Wakili wa wananchi hao Jebrah Kambole amesema mashauri hayo ya Kikatiba ni namba 4 na 6 ya 2018 ambapo yamepangwa kusikilizwa April 5,2018.

Wakili Kambole amesema mahakama hiyo ilipanga kuanza kusikiliza mashauri hayo leo March 9, lakini imeshindikana kwa sababu baadhi ya majaji wamepangiwa kesi nyingine.

Wakili Kambole amesema kuwa mahakama imemuamuru AG kuwasilisha majibu yake kuhusu mashauri hayo March 21,2018.

“Mashauri haya ya yanapinga sheria mbalimbali ikiwemo kupinga sheria ya uchaguzi, pia Wakurugenzi wa Halmashauri kuwa wasimamia wa Uchaguzi wakati inapaswa kuwepo tume huru ya Uchaguzi,”alisema Wakili Kambole.

Wakili Kambole amesema kwenye shauri namba 4 wananchi hao 28 wanapinga sheria za Jeshi la Jeshi la Polisi na vyama vya siasa ambazo zinatoa muongozo wa kuzuia mikutano ya Kisiasa na kusababisha madhara mengi kwa wananchi.

“Hivyo kimsingi tunapinga sheria hizo ambazo ni kandamizi na zinakiuka misingi ya Katiba, ibara ya 18 Uhuru wa kujieleza kufanya mamuzi juu ya maisha ya Watanzania na nchi,” alisema Wakili Kambole.

Pia sheria hizo zinakiuka haki ya kusikilizwa kwa watu wanaotoa taarifa kwa Jeshi la Polisi wakitaka kuandamana wanapata amri kabla ya kusikilizwa, hivyo kimsingi tunaangalia uhalali wa hizo sheria kwa Katiba yetu ya Tanzania.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 16 inatoa majibu kwa mtu yoyote anayeona sheria imekiukwa ana wajibu wa kuleta shauri Mahakamani.

Mahakama imeyapanga mashauri hayo kuanza kutajwa April 5, 2018.

No comments:

Post a Comment

Popular