Mkuu wa mkoa wa Manyara awaonya Tarura. - KULUNZI FIKRA

Friday 2 March 2018

Mkuu wa mkoa wa Manyara awaonya Tarura.

 
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ameagiza Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), kuwashirikisha viongozi wa maeneo husika pindi wanapotaka kuandaa bajeti za barabara ili kutosababisha migongano ya kutotambulika barabara zinazopaswa kupewa kipaumbele kwenye ukarabati na ujenzi.

Akizungumza jana, mjini Babati kwenye kikao cha bodi ya barabara ya mkoa huo, Mnyeti amesema Tarura ni chombo cha Serikali, hivyo wanatakiwa wawashirikishe viongozi wa maeneo husika ili kusiwapo na migongano tofauti na sasa kwani wanajitenga.

Mnyeti amesema Tarura wasijigeuze kuwa taasisi ya kipekee iliyopo Serikali Kuu ambayo haiwajibiki wilayani au mkoani ilhali ni wajibu wao kutoa taarifa na kushiriki vikao.

"Hizo barabara siyo za kwenu, sitaki kusikia mnapitisha barabara zijengwe ilhali viongozi wa wilaya hawajui au mimi sijui, ninyi Tarura msigeuze taasisi kuwa ya kwenu," amesema Mnyeti.

Amesema kwenye mkoa wake hataki ubabaishaji hivyo atamchukulia hatua kali meneja yeyote wa Tarura ambaye anafanya kazi kwa mazoea badala ya kushirikisha viongozi wa maeneo husika.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa amesema wanasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 1,656 na madaraja 217, kati ya hizo kilometa 206 ni barabara kuu na kilometa 1,449 ni barabara za mkoa.

"Hali ya barabara ni ya kuridhisha ingawa kuna baadhi zinapitika kwa shida wakati wa mvua hususani zilizopandishwa daraja mwaka 2009 kutoka kuwa za wilaya hadi kuwa za mkoa," amesema mhandisi Rwesingisa.

Ametaja baadhi ya barabara zilizoathirika na mvua zilizonyesha hivi karibuni ni Mbuyu wa Mjerumani-Mbulu, Kibaya-Dosidosi, Kilimapunda-Kidarafa, Losinyai-Njoro, Mogitu-Haydom na Singe-Kimotorok-Sukuro.

Meneja wa Tarura Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Martin Mwashambwa amesema wilaya hiyo ina mtandao wa barabara wenze kilometa 1,373.68.

Mhandisi Mwashambwa amesema barabara za wilaya ni kilometa 932. 58 barabara za vijiji kilometa 327.96 na barabara za miji ni kilometa 137.14.

No comments:

Post a Comment

Popular