Mary Nagu amekamatwa na Jeshi la polisi. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 8 March 2018

Mary Nagu amekamatwa na Jeshi la polisi.

 
Mbunge wa Hanang kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe  Mary Nagu jana aliangukia mikononi mwa Polisi baada ya kukamatwa akiwa jimboni kwake katika kijiji cha Lalaj Kata ya Lalaj wilayani Hanang.

Mhe Nagu alikamatwa majira ya saa 11:00 jioni kufuatia agizo la mkuu wa Wilaya ya Hanang Sara Ally Msafiri kwa madai kuwa Mbunge huyo alitofautiana maagizo na mkuu huyo wa Wilaya.

Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya Sarah Msafiri ameeleza kuwa ameagiza kukamatwa kwa Mbunge huyo baada ya kuchoka kumvumilia kutokana na kauli anazozitoa kwenye mikutano yake na wananchi akihamasisha wasishiriki shughuli za maendeleo.

Pia amemtuhumu Mbunge huyo kuwataka wananchi wasishirikiane naye jambo ambalo alidai ni sawa na kuwataka wananchi wasishirikiane na serikali kwa sababu yeye anasimama kama serikali

“Ni kweli tumemkamata na sababu kubwa ni kuhamasisha wananchi wasishiriki shughuli za maendeleo na pia anawataka wananchi wasishirikiane na Mimi wakati anajua Mimi nasimama kama serikali” alisema mkuu wa Wilaya  Sarah Msafiri.

Hata hivyo Mhe Nagu aliachiwa jana hiyo hiyo baada ya uongozi wa CCM Wilaya ya Hanang kuingilia kati kutafuta suluhisho la mvutano huo ambao haujaelezwa ulikuwa unahusu nini haswa.

Jitihada za kuwatafuta pande zote mbili kwaajili ya kupata ufafanuzi zaidi bado zinaendelea lakini simu zao hazipokelewi, endelea kufuatilia tutakufahamisha.

No comments:

Post a Comment

Popular