Makonda afunguka kuhusu Wananchi wa Dar es salaam. - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 6 March 2018

Makonda afunguka kuhusu Wananchi wa Dar es salaam.

 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ameitaka bodi ya barabara kuhakikisha fedha za Mkopo wa Ujenzi wa Miundombinu ya Barabara DMDP zinatumika kujenga Barabara za kisasa na sio kutumika kwenye Warsha, Semina na Safari za Mafunzo Nje ya Nchi ambapo Mwisho wa siku fedha hiyo inamalizika bila kufanya jambo lililokusudiwa.

Makonda amesema Dar es salaam ina fedha za DMDP takribani Billion 600 kwaajili ujenzi wa Barabara na Mifereji ya Maji lakini asilimia kubwa ya fedha hizo zimekuwa zikitumika kwenye semina na Safari za Nje ya Nchi kujifunza namna ya usimamizi wa Barabara jambo linalopelekea Serikali kulipa madeni kwa miradi ambayo haijatekelezwa.

Aidha Makonda amesema kuwa amegundua gharama ya kujenga Barabara ya Kilometa moja kwa fedha ya DMDP ni sawa na gharama ya kujenga barabara ya TANROAD Kilometa 3 hivyo ameshauri kikao hicho kuangalia kwa umakini jambo hilo ili fedha hizo ziweze kuleta tija kwa wananchi kwa uwepo wa barabara zenye ubora.

Makonda amesema kwa mwaka wa fedha wa 2018-2019 Mkoa wa Dar es salaam umetenga kiasi cha shilingi Billion 289.3 kwaajili ya matengenezo ya barabara kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini TARURA,  TANROAD na vyanzo vya ndani vya Halmashauri.

Makonda amesema hataki kuona Wananchi wa Dar es salaam wanateseka kutokana na ubovu wa barabara zenye Mashimo na mahandaki jambo linalopelekea hasara ya uharibifu wa vyombo vya usafiri na wakati mwingine ongezeko la msongamano wa magari.

Aidha Makonda ameanza kuona nuru baada Wakandarasi wa barabara za Dar es salaam kuanza kufuata taratibu kwa kutengeneza barabara za kisasa na kuwasihi TARURA wawe wasimamizi wazuri wa Ujenzi Barabara Kama wanavyofanya TANROAD ili tuwe na barabara zinazodumu muda mrefu.

No comments:

Post a Comment

Popular