Mahakama ya Afrika ya Haki za binadamu yaibuka na Kesi ya Babu Seya. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 22 March 2018

Mahakama ya Afrika ya Haki za binadamu yaibuka na Kesi ya Babu Seya.

 
Wakati mwanamuziki Nguza Viking (Babu Seya) na mwanawe Johnson Nguza (Papii Kocha) wakiwa nje kwa msamaha wa rais, Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), imeahirisha kutoa hukumu ya maombi waliyofungua kupinga kifungo cha maisha jela.

Babu Seya na Papii Kocha waliachiwa kwa msamaha wa rais Desemba 9, mwaka jana kutokana na kifungo cha maisha jela walichohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Juni mwaka 2004 baada ya kumkuta na hatia ya kunajisi na kulawiti watoto 10 ambapo walikata rufaa Mahakama za juu na kugonga mwamba na hivyo kulazimika kukimbilia AfCHPR wakidai haki zao zilivunjwa.

Akiahirisha kesi hiyo Rais wa AfCHPR, Jaji Sylvaine Ore kutoka nchini Ivory Cost, amesema wamelazimika kuahirisha kusoma hukumu hiyo hadi Ijumaa Machi 23, kutokana na upande wa waomba maombi kutofika mahakamani.

Katika shauri hilo Jamhuri iliwakilishwa na Mwanasheria wa Serikali Mkuu Sara Mwaipopo akisaidiana na Mwanasheria wa Serikali Mkuu Nkasori Sarakikya.

Hata hivyo, Mwanasheria Daniel Kalasha akitoa maoni yake kuhusiana na hukumu hiyo amesema vyovyote itakavyokuwa hukumu hiyo haiwezi kuathiri msamaha wa rais waliopata waomba maombi hao lakini walipaswa kuitaarifu mahakama kuachana na kesi hiyo kutokana na sababu hizo.

Amesema utaratibu ulivyo wao ndiyo walifungua hiyo kesi baada ya kuona wamepata msamaha wa rais walikuwa wanapaswa waiandikie barua mahakama kwamba wameshapata msamaha huo hivyo wanaomba mahakama isitoe hukumu.

“Lakini kama hawakufanya hivyo mahakama itaendelea na kazi yake kama kawaida na aidha itawakuta na hatia au isiwakute na hatia kwamba jambo lao limeshapata msamaha na msamaha wa rais huwezi kuuhoji popote, hakuna mwenye mamlaka ya kuhoji kwa sababu kile kifungo kimeshabatilishwa tayari", alisema Wakili Kalasha.

“Kesi ingekuwa bado inaendelea msamaha ukatoka basi wakili ndiyo alikuwa na wajibu wa kuiambia mahakama hatuna nia tena ya kuendelea na rufaa yetu kwa hiyo kesi inakuwa imekufa", alisema Wakili Kalasha.

“Lakini hata hivyo halina uzito tena hata kama wakikutwa na hatia tayari wameshapata msamaha wa rais ambao uko kwa mujibu wa katiba,” alisema Wakili Kalasha.

Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu (AfCHPR) kesho Ijumaa Machi 23, 2018 itasoma hukumu ya kesi ya wanamuziki wa dansi, Nguza Viking maarufu Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’.

Wanamuziki hao walikata rufaa iliyosajiliwa na kupewa namba 006/2015 katika mahakama hiyo kupinga kifungo cha maisha.

Wakati hukumu hiyo ikitarajiwa kusomwa kesho, Babu Seya ambaye ni mtunzi wa kibao maarufu cha “Seya” na Papii Kocha ambaye wameshirikiana katika wimbo huo ni miongoni mwa wafungwa 8,157 waliosamehewa na Rais John Magufuli siku ya Uhuru wa Tanganyika, Desemba 9, 2017.

Walikuwa kati ya wafungwa 61 waliokuwa na adhabu za vifungo vya maisha na kunyongwa ambazo si rahisi kupata msahama wa kawaida wa mkuu wa nchi unaotolewa siku ya sherehe hizo.

Rais wa mahakama hiyo, Jaji Sylvian Ore alisema itasoma hukumu hiyo baada ya kukamilisha mahitaji yote na kupata taarifa za wakata rufaa.

Hata hivyo, wakati Jaji Ore akiahirisha kusoma hukumu hiyo, wanamuziki hao hawakuwepo mahakamani.

Baadhi ya mawakili waliokuwepo mahakamani hapo wamesema licha ya kuwa wanamuziki hao wamepata msamaha wa rais, hukumu yao itasomwa.

"Mahakama hapa itatoa hukumu ili kuweka rekodi za kimahakama katika kesi za aina hii na hata kama ikieleza walikuwa na hatia haina athari kwao,” amesema wakili Daniel Kalasha.

Katika kesi hiyo, Jamhuri inawakilishwa na mawakili Sara Mwaipopo na Nkasori Sarakikya.

No comments:

Post a Comment

Popular