Laini za simu zavunja rekodi nchini - KULUNZI FIKRA

Thursday 1 March 2018

Laini za simu zavunja rekodi nchini

 
Laini za simu za mikononi zimeongezeka kutoka 2,198 mwaka 1995 hadi kufi kia zaidi ya milioni 40 ilipofi ka Desemba mwaka jana, ambazo zipo mikononi mwa watu na hivyo kuendeleza ustawi wa Watanzania.

Katika hatua nyingine, serikali imezindua mfumo wa kusajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole (biometria), ambao utadhibiti changamoto za usajili zilizopo. Changamoto hizo ni pamoja na udanganyifu unaofanyika sasa kwa kutumia laini za sasa, sambamba na kuisaidia serikali kuwa na takwimu sahihi ya watumiaji wa huduma za simu za mkononi, zitakazosaidia kuweka mipango ya uchumi wa Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt Maria Sasabo, Mwakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Kitolina Kippa alisema ongezeko hilo kubwa na la haraka la laini za simu, limekuja baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa utoaji wa leseni unaozingatia mwingiliano wa teknolojia mwaka 2005. “Natoa mwito kwa wananchi kuzingatia sheria kuhusu matumizi halali ya huduma za mawasiliano, ikiwa ni pamoja na umuhimu wa usajili laini za simu,” alisema.

Akizungumzia usajili wa laini za simu kwa kidole, Kippa alisema utafanyika kwa majaribio katika mikoa sita nchini. Alisema pamoja na kuwepo matumizi sahihi ya simu za mkononi, lakini bado kuna watumiaji wachache ambao wanatumia huduma za mawasiliano vibaya. “Hawa wanatumia mianya katika usajili wa laini za simu kujipatia laini ambazo zimesajiliwa kwa majina bandia au ambazo hazijasajiliwa.

Wapo wanaotumia simu za mkononi kutuma ujumbe wa kashfa, matusi, kejeli, maudhi, dhihaka na unyanyapaa,” alisema. Alisema mfumo huo wa usajili ni hatua muhimu ya matumizi ya teknolojia katika kudhibiti changamoto za usajili na kuwezesha watoa huduma, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na serikali kuwa na takwimu sahihi za watumiaji wa huduma za simu za mkononi na vifaa vingine vya mawasiliano vinavyotumia laini za simu. Pia alisema kuwepo kumbukumbu sahihi za laini za simu, kutafanikisha kuanzishwa na kuwekwa kwa Kanzi Data ya laini za simu zilizosajiliwa ambayo inatakiwa na TCRA.

“Usajili sahihi pia ni muhimu kwa watumiaji wa huduma na wateja wa bidhaa kujihakikishia usalama wa kutotapeliwa au kuibiwa mitandaoni. Usajili wa laini za simu unawalinda watumiaji dhidi ya wahalifu wanaotumia mitandao,” alisema. Alisema; “Serikali tunafurahi tunapoona na kushuhudia ubunifu na utekelezaji wa mipango ambayo inalenga kuhakikisha maendeleo ya sekta na uchumi wa nchi kwa ujumla na ambayo inawahakikishia wananchi usalama wao na faida za kiuchumi na kijamii wanapotumia mitandao ya simu,” alisema.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema kuwa mfumo huo wa usajili wa kutumia biometria umeanza kwa majaribio katika mikoa sita ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, Iringa, Tanga, Singida na Mjini Magharibi na watakapokamilisha wataendelea na mikoa mingine. “Ili kukabiliana na changamoto za usajili, TCRA, watoa huduma za simu za mkononi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) tuliazimia kuja na mfumo huu wa usajili wa laini za simu hapa nchini ili kuepuka udanganyifu na kudhibiti uhalifu,” alisema.

Pia alisema usajili huo, utarahisisha huduma za kuhamia mtandao mwingine wa simu za mkononi, bila kubadili namba ya simu na utawawezesha watoa huduma kuwajua wateja wao na hivyo kuwahudumia kwa ufanisi zaidi. Hata hivyo, alisema TCRA imeandaa mpango mkubwa wa kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kusajili laini za simu kwa utaratibu uliowekwa kisheria.

No comments:

Post a Comment

Popular