Kauli ya Dkt Kigwangalla yaibua Mijadala. - KULUNZI FIKRA

Monday, 5 March 2018

Kauli ya Dkt Kigwangalla yaibua Mijadala.

Kauli ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamisi Kigwangalla kutaka mitumbwi ya raia wa kigeni wanaoingia pori la akiba la Kimisi na Burigi mkoani Kagera kuzamishwa majini ili warejee walikotoka wakiogelea imeibua mjadala katika mitandao ya kijamii, huku baadhi wakisema inachochea vurugu.

“Kuzamisha mitumbwi si kuruhusu kuua. Ni kutuma salamu kuwa huku Tanzania si shamba la bibi, ni nchi ya watu na inapaswa kuheshimiwa. Hatutawaua kama wao wanavyofanya, lakini tuna hakika atakayeogelea na kufika salama kule kwao atafikisha salamu zetu kuwa Tanzania si pa kwenda kuchezea tena,” alisema Dkt  Kigwangalla jana alipoulizwa na Mwananchi juu ya kauli yake iliyozua mjadala aliyoitoa juzi.

Mapori ya Kimisi, Burigi na Biharamulo yapo mkoani Kagera na yanatenganishwa na Mto Kagera na nchi ya Rwanda.

Waziri huyo juzi aliweka picha ya video katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter ikimuonyesha akitoa maagizo kwa maofisa na watendaji wa wizara kuhusu hatua wanazopaswa kuchukua dhidi ya wageni wanaovamia hifadhi hiyo.

Katika maagizo hayo alisema, “…. kama wao wanaua watu wetu na sisi mnajua la kufanya. Maana hatuwezi kuonekana sisi wajinga wao wajanja. Hakuna ujirani mwema wa aina hiyo kwani ninyi mnashindwa kuzamisha mitumbwi yao, kitu gani kinashindikana?”

“Mtu anayevuka akija upande wetu mnazamisha mitumbwi, mnawapoteza. Mkipoteza wawili, watatu mnawarudisha warudi kwa kuogelea, wakifika kwao hakuna atakayerudi huku. Tutume salamu kwamba na sisi hatuchezewi.”

Mmoja wa waliohoji kauli ya waziri huyo ni mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro, “Nilitamani kusikia waziri akimuagiza mkuu wa polisi kuwakamata wauaji ndani ya siku saba. Nilitamani kusikia kuwa hao wanaovuka na kuingia kwenye hifadhi yetu inaagizwa wakamatwe mara moja na kufikishwa mahakamani si kusikia nao wauawe.”

Lakini, jana katika ufafanuzi wake kuhusu kauli yake ya juzi, Dk Kigwangalla aliliambia Mwananchi kuwa muda wa kuwavumilia wageni hao sasa umefikia mwisho.

“Nilichokisema ni kwamba, wenzetu upande wa pili wa Mto Kagera ambao ndiyo mpaka, wana hifadhi yao inayoitwa Akagera, na sisi huku upande wetu tuna hifadhi ya Kimisi. Ya kwao wanailinda kwa mtutu wa bunduki, na Watanzania wengi tu wameuawa wakienda kuvua samaki Ziwa Ihema lililoko upande wao wa hifadhi. Sisi hatuui watu wao waliovamia upande wetu wa hifadhi,” alisema  Dkt Kigwangalla.

“Tunawaondoa kistaarabu. Hakuna ujirani mwema wa wao kuua watu wetu wanaovuka upande wao kuvua samaki huku sisi tukiwalea watu wao wanaokuja kulima ndani ya hifadhi yetu ya Kimisi, wanavuna mbao, wanafanya uwindaji haramu kwenye hifadhi yetu.”

Alisema kwa sasa wataimarisha ulinzi wa mapori ya Tanzania, kuanza kuondoa mifugo yote iliyosalia, kufyeka mazao na kuondoa wavamizi wote.

“Sasa kama kuna mtu atavuka na mtumbwi wake kuja kwetu baada ya hapo tutamnyang’anya mtumbwi wake na kumtaka arudi alikotoka kwa kuogelea,” alisisitiza.

Alisema wafugaji kutoka nchi jirani, wameigeuza Tanzania kama shamba la bibi kwa kulisha mifugo yao hadi maeneo ya hifadhi.

“Uchungu na hasira ya kudharauliwa na kuchukuliwa poa ilinipelekea kutoa maneno makali. Na nimefurahi kuyasema maana nimepata nafuu moyoni,” alisema Dk Kingwangalla.

Alisema ana taarifa watu wamekwenda hifadhi za Makere, Ugalla, Katavi na Malagarasi.

No comments:

Post a Comment

Popular