Jeshi la polisi: Watakaoandamana April 26 watajikuta na vilema. - KULUNZI FIKRA

Friday, 23 March 2018

Jeshi la polisi: Watakaoandamana April 26 watajikuta na vilema.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Gilles Muroto akizungumza na Yuda Mbata ambaye anatuhumiwa kuhamasisha maandamano kwenye mitandao ili wananchi waandamane April 26 mwaka huu. Watu wawili walikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma hiyo.

Wakati vuguvugu la maandamano yanayoandaliwa kupitia mitandao ya kijamii likiendelea kupamba moto, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema watakaoandamana siku hiyo watapata matatizo makubwa na wengine watajikuta wakiwa na vilema.

Kamanda Muroto aliyasema hayo Juzi alipowafikisha mbele ya wanahabari, watu wawili akiwamo dereva wa Mfuko wa Bima ya Taifa (NHIF), Amandus Manchali (31) mkazi wa Kigamboni Geti Jeusi jijini Dar es Salaam na Yuda Mbata (29) mkulima na mkazi wa Bahi.

Muroto alisema watu hao walikuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuhamasisha maandamano yenye chuki na viashiria vya kuvuruga amani ya nchi.

“Watakaoingia barabarani siku hiyo, watapata matatizo makubwa kwani wengine watajikuta wakiwa vilema na ni vizuri wakaitumia mitandao katika kuhamasisha shughuli za maendeleo badala ya kuhamasisha ujinga,” alisema Muroto.

Alisema kuna watu wasiopenda amani na utulivu wa nchi, wanatumia vibaya mitandao ya mawasiliano kuvunja sheria kwa kuhamasisha chuki dhidi ya Serikali na kuhamasisha maandamano yasiyo halali.

“Hawa watu ni sawa na watu walioshiba ambao hawajui nchi imetoka wapi na mtu akishiba akavimbiwa anaweza kuhamishia choo ndani,” alisema kamanda Muroto.

Wakati hayo yakiendelea Dodoma, taarifa zilizopatikana huko Moshi zinadai kuwa mfanyabiashara mashuhuri anayemiliki maduka ya kuuza vifaa vya elektroniki ya Mekus Electronic, Ladislaus Moshi, alikamatwa Jumamosi iliyopita na kusafirishwa mpaka Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah Jana alithibitisha kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo, lakini akakataa kuingia kwa undani akisema suala hilo linachunguzwa na Polisi jijini Dar es Salaam.

Kamanda Issah alifafanua kuwa mtuhumiwa huyo alisafirishwa kwenda Dar es Salaam na kumwelekeza mwandishi wetu kuwasiliana na makao makuu ya Polisi Dar es Salaam ambako uchunguzi wa tuhuma zake unafanyika.

Makamanda wazungumzia maandamano Aprili 26

Wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma akitoa onyo kali, makamanda wa Polisi katika mikoa mbalimbali nchini wamesema yeyote atakayebainika kuingia barabarani siku hiyo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Wamesema wanaendelea na uchunguzi kuwabaini watakaofanya hivyo huku wakiwatoa hofu wananchi wakiwataka waendelee na shughuli zao za kiuchumi.

Akizungumza na kulunzifikra blog, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema wanaendelea kufanya upelelezi kuhusu jambo hilo.

“Kwa hiyo siwezi kukuambia kama tumewakamata au lah, jambo hili bado tunaendelea kulifanyia upelelezi lakini tu niseme, ole wake atakayekutwa anahamasisha maandamano,” alisema kamanda Msangi.

Alisema Mtanzania mwenye akili timamu na anayetanguliza uzalendo wa nchi yake mbele hawezi kuhamasisha maandamano ambayo madhara yake makubwa ni kuvuruga amani ya nchi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga alisema uhamasishaji wa maandamano hayo unafanywa kwenye mitandao pekee.

Alisema intelijensia inaendelea kuwasaka watu au vikundi vinavyojipanga kwa jambo hilo au kuendelea kuhamasisha maandamano hayo kinyume cha sheria.

“Huku Mkoa wa Mbeya hatujamkamata mtu ‘phyisically’ akihamasisha upuuzi huu wa maandamano na niwaombe wakazi wa mkoa huu waendelee na kazi zao kama kawaida, wasikubali kabisa kuandamana au kuhamasisha jambo hili,” alisema kamanda Mpinga.

Alisema wengi wanaohamasisha suala hilo mitandaoni wanatumia majina bandia na wanaendelea kusakwa.

“Kwa hiyo mtu yeyote atakayeingia barabarani siku hiyo, polisi tutafanya kazi yetu kuhakikisha mkoa unaendelea kuwa wa amani na utulivu,” alisema Kamanda Mpinga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Jumanne Murilo alisema tayari viongozi mbalimbali walishazungumzia suala hilo ambalo kwa sasa hataweza kulielezea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jinathan Shanna alisema kama ilivyo kwenye mikoa mingine, polisi wa mkoa huo hawajalala.

Kamanda Shanna alisema walichobaini ni kwamba wapo wanaofanya hivyo kwa kutojua sheria ya mitandao ambao hata hivyo, hawatakuwa na msamaha kisheria.

“Kuna watu wanapokea ujumbe wa kuhamasisha maandamano halafu wanausambaza, sasa sijui wanafanya hivyo kwa sababu ya ubwege wao wa kutokujua au wana lengo la kuhamasisha hata kama wanajua kufanya hivyo ni kosa, nawasihi waache mara moja,” alisema Kamanda Shanna.

Aliwataka wakazi wa mkoa huo kutokubali kusambaza ujumbe wa aina yoyote ile wenye lengo la kuvuruga amani, badala yake wafute au kubaki nao wao wenyewe.

Kamanda wa Polisi wa Temeke, Emmanuel Lukula alisema Jeshi hilo pia linaendelea kuwasaka watu hao na kwamba wakibaini uwepo wa harufu yoyote wahusika hawataachwa, watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

“Viongozi walishatoa maelekezo na sisi tunatekeleza kwa hiyo niwaambia tu wananchi kwamba, polisi hatujalala, ninachohamasisha waendelee kufanya kazi zao za kimaendeleo kama kawaida,” alisema kamanda Lukula.

“Waachane kabisa na jambo hili, watii sheria bila shuruti, lakini kwa atakayependa kushurutishwa, basi sheria itachukua mkondo wake", alisema kamanda Lukula.

No comments:

Post a Comment

Popular