Jeshi la polisi limefafanua kuhusu uchunguzi wa wa tukio la afisa wa ubalozi wa Syria. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 21 March 2018

Jeshi la polisi limefafanua kuhusu uchunguzi wa wa tukio la afisa wa ubalozi wa Syria.

 
Jeshi la Polisi Jijini Dar es Salaam linamshikilia mfanyakazi wa ubalozi wa Syria akihusishwa na tukio la kushambuliwa, kuibiwa takribani Euro 93,000 Mhasibu wa Ubalozi huo nchini Tanzania siku ya Jana.

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, RPC Muliro Jumanne Muliro wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Leo  Machi 21, 2018  baada ya kupita takribani siku tatu tokea lilipofanyika tukio la kushambuliwa mhasibu wa Ubalozi wa Syria kwa kutumia nondo na kufanikiwa kuiba fedha alizokuwa anazipeleka kuzihifadhi katika moja ya benki na kutoroka na dereva aliyekuwa anaendesha gari hilo.

"Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali na likafanikiwa kulipata gari alilokuwa akitubia Balozi likiwa limetelekezwa eneo la Msasani eneo la bonde la Mpunga Jijini Dar es Salaam ambapo limekutwa limefungwa lakini dereva aliyekua amekula njama na wale waharifu alikuwa ameshatokomea", amesema kamanda Muliro.

Pamoja na hayo, kamanda Muliro ameendelea kwa kusema "upelelezi juu ya shauri hili linaendeelea na Polisi wanafanya kila wawezalo kwa kushirikiana na idara mbalimbali za Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba waharifu wote waliokula njama wanakamaatwa na hatua za kisheria kuchukuliwa.

"Kwa kifupi tukio hili limegubikwa na njama za moja ya mtumishi aliyeajiriwa na ubalozi wa Syria na hatimaye kufanyakazi na mharifu bila ya kujitambua,  mtuhumiwa mmoja ambaye ametokana na sababu za kiuchunguzi anashikiliwa na Jeshi la Polisi na nina uhakika atatusaidia kupatikana kwa waharifu wote walitumika katika tukio hili wanakamatwa", alisema kamanda Muliro.

Kwa upande mwingine,  kamanda Muliro ametoa wito kwa mashirika ya umma na yasiyokuwa ya umma kuwa makini pindi wanapotoa ajira kwa watumishi pindi wanapotaka kuwapa ajira katika maofisi yao ili kuweza kujikinga na kumuajiri mtu ambaye ni mwizi kwa namna moja ama nyingine.

No comments:

Post a Comment

Popular