Fatma Karume: Nina Baraka zote za Tundu Lissu kugombea Urais TLS. - KULUNZI FIKRA

Saturday, 24 March 2018

Fatma Karume: Nina Baraka zote za Tundu Lissu kugombea Urais TLS.

Wakili wa kujitegemea, Fatma Karume, amesema ana baraka za Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Mhe Tundu Lissu, kugombea urais katika chama hicho baada ya muda wa mwanasheria huyo machachari kwisha.

Uchaguzi wa TLS unatarajia kufanyika Aprili 14, ambapo  Mhe Tundu Lissu aliye kwenye matibabu nchini Ubelgiji, hatagombea tena baada ya kumaliza mwaka mmoja wa uongozi wake.

Kutokana na kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka Jana na kukaa kwenye matibabu nje ya nchi kwa muda mrefu, Mhe Tundu  Lissu anakuwa ametumikia nafasi yake kama Rais wa TLS kwa miezi sita pekee.

Akizungumza na kulunzifikra blog  ofisini kwake Jana, Fatma ambaye pia ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, alisema mwanzoni hakuwa tayari kugombea urais wa TLS lakini baadaye akashawishiwa na mawakili vijana akakubali.

“Yalikuwa maamuzi magumu sana kwa sababu sikutaka, nilikuwa naombwa na vijana kwamba Fatma chukuwa fomu ugombee tutakuchagua nikasema hapana nina majukumu mengi", alisema Wakili Fatma Karume.

“Nakumbuka ilipofika Alhamisi kuna kijana mmoja akanifuata akaniambia nakuomba uchukue fomu nikamwambia siko interested kwa sababu nilikuwa nataka nijipunguzie majukumu", alisema Wakili Fatma Karume.

“Sasa baadaye nilivyojiuliza kujipunguzia huku majukumu ina maana nafikiria watu au mimi mwenyewe nikasema huu utakuwa ubinafsi…baada ya kutafakari nikamtumia message yule kijana kwamba achukue fomu ajaze na sehemu ya wadhamini halafu aniletee nisaini", alisema Wakili Fatma Karume.

“Ujue nilikuwa siamini kama atafanya hivyo, lakini ilipofika Ijumaa namwona yule kijana anafika ofisini kwangu na fomu pamoja na sehemu ya wadhamini isipokuwa sehemu yangu, hivyo nikajaza na kusaini sasa mtu kama huyo utamwangusha kweli,” alihoji Wakili  Fatma Karume.

Mwanasheria huyo alisema baada ya kujaza fomu akampigia simu Mhe Tundu Lissu na kumweleza kuhusu hilo na akapata baraka zote.

“Nadhani kila mtu anajua kuwa Lissu ni rafiki yangu na ninampenda sana na nikizungumza naye napata faraja, napata furaha, huwa tunataniana sana. Hivyo baada ya kujaza fomu nikampigia kumshirikisha na akanipa baraka zote", alisema Wakili Fatma Karume.

“Ilikuwa lazima nizungumze na  Mhe Tundu Lissu kwa sababu yaliyotokea mnayajua, urais wake ulikatishwa katikati na hajaweza kutimiza yale aliyoahidi kuyatimiza, hivyo kitu kama hicho kimemtokea mwenzako na unagombea lazima uzungumze na mwenzako upate baraka,” alisema wakili huyo", alisema Wakili Fatma Karume.

No comments:

Post a Comment

Popular