Club ya Simba yafafanua mchakato wa kumkabidhi timu Mo Dewji ulipofika. - KULUNZI FIKRA

Saturday 3 March 2018

Club ya Simba yafafanua mchakato wa kumkabidhi timu Mo Dewji ulipofika.

 
Uongozi wa klabu ya Simba umesema kuwa iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mazungumzo na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji "Mo" kwa ajili ya kuwekeza katika klabu hiyo yenye makao yake makuu Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah, alisema kuwa Mo ameridhia maelekezo mapya yaliyotolewa na serikali ambayo yanahitaji mwekezaji apewe kiasi cha asilimia 49 na wanachama wabakie na asilimia 51.

Salim alisema kuwa katika kuhakikisha zoezi hilo linakwenda vizuri, tayari wameshasaini mikataba ya awali ambayo inapelekea kurahisisha mchakato huo ambao utabadili mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1936.

"Tumefikia hatua nzuri katika mchakato huu, kuna baadhi ya nyaraka ambazo zimeshasainiwa, lakini kwa sasa macho na masikio yetu yako kwenye kuelekeza nguvu katika mechi ngumu zinazotukabili," alisema kwa kifupi Salim.

Kuhusu suala la uwanja, kiongozi huyo ambaye alikutana na waandishi wa habari jana asubuhi alisema kuwa wanatarajia kuzipata nyasi bandia zilizokuwa zimezuiwa bandarini wakati wowote kuanzia sasa na mchakato wa ujenzi utaanza hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment

Popular