Watuhumiwa nane kati ya kumi na moja wa mauaji ya mwanafunzi wa shule ya Scolastica waachiwa Uhuru. - KULUNZI FIKRA

Tuesday 13 February 2018

Watuhumiwa nane kati ya kumi na moja wa mauaji ya mwanafunzi wa shule ya Scolastica waachiwa Uhuru.

WATUHUMIWA wanane kati ya 11 walioshikiliwa na jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Scolastica iliyopo katika Mji mdogo wa Himo mkoani Kilimanjaro,Humphrey Makundi (16) wameachiliwa huru.

Miongoni mwa watuhumiwa hao ni wale waliotajwa kushiriki katika kuficha taarifa juu ya kifo cha mwanafunzi huyo akiwemo Daktari wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi na askari wa kitu cha polisi Himo .

Daktari huyo ndiye anayetajwa kuupokea mwili wa marehemu na kuufanyia uchunguzi na kisha kuruhusu uzikwe haraka ndani ya siku mbili baada ya kufikishwa huku akiwaleza ndugu wa marehemu taarifa zisizo za kweli kwamba mwili uliozikwa ulikuwa ni wa mzee na si mtoto.

Hadi sasa ni watuhumiwa watatu wamefikishwa mahakama ya hakimu mkazi Moshi na kusomewa shitaka moja la mauaji ya kukusudia akiwemo mmoja wa wakurugenzi wa shule ya Scolastika, Edward Shayo (63) , mlinzi wa shule hiyo ,Hamis Chacha (28) na Labani Nabiswa(37) ambaye ni makamu mkuu wa shule hiyo.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro,Koka Moita amesema kuwa ,watuhumiwa wanane waliokuwa wakishikiliwa na jeshi la polisi kwa uchunguzi kutokana na tuhuma hizo za mauaji waliachiliwa huru baada ya uchunguzi wa Kina kuhusiana na mauaji hayo.

“Baada ya uchunguziwa kina kuhusiana na watuhumiwa hao, wameonekana hawana hatia yoyote hivyo jeshi la polisi halikuwa na sababu ya kuendelea kuwashikilia.”alisema Koka Moita .

Kuhusu malalamiko ya baadhi ya mahabusu wanaowalalamikia polisi kufanya upendeleo wa kutomfunga pingu mshitakiwa wa pili na mmoja wa wakurugenzi wa shule ya Scolatica,Edward Shayo,kamanda Koka ametetea hatua hiyo.

Alisema si lazima washitakiwa ama watuhumiwa kufungwa pingu na kuongeza kuwa jeshi la Polisi huchukua hatua hizo kwa watuhumiwa ama washitakiwa wanaoonekana kuwa na dalili za ukorofi.

“Kama unaona mtuhumiwa ana kutoroka,hapo ndiyo tunachukua hatua za kumfunga pingu lakini si kila mtuhumiwa anaweza akafungwa pingu”,alisema Moita.

Alisesema kuwa,wapo watuhumiwa ama washitakiwa ambao hawapaswi kufungwa pingu wakiwamo watoto wadogo pamoja na wenye umri mkubwa au wazee na kwamba mshitakiwa wa pili katika shauri hilo la mauaji Edward Shayo yupo kwenye kundi la wazee akiwa na umri wa miaka 63.

Wakati kamanda Koka akitetea hatua ya mshitakiwa huyo kutokufungwa pingu,Novemba 11 mwaka jana mshtakiwa huyo alipofikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo alifungwa na wenzake .

Shauri hilo lililo mbele ya Hakimu Mkazi ,Julieth Mawole lilitajwa kwa mara ya kwanza Novemba 11 mwaka jana ambako washitakiwa hao walisomewa shitaka lao na mawakili wa serikali Kassim Nassir akisaidiana na wakili mwenzake,Faygrace Sadallah huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Elikunda Kipoko .

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa mahakamani hapo ,washitakiwa hao wanadaiwa kuwa mnamo Novemba 6 mwaka jana kwa pamoja walimuua kwa kukusudia mtu aitwaye Humphrey Makundi.

Hata hivyo washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji hadi mahakama kuu


TUKIO LILIVYOKUWA

Novemba 6 mwaka jana marehemu aliyekuwa mwanafunzi wa bweni katika shule hiyo ya sekondari ya Scolastica iliyopo katika mji mdogo wa Himo wilaya ya Moshi Vijijini,alitoweka shuleni hapo.

Hata hivyo,Novemba 10 mwaka jana mwili wake uliokotwa ndani ya Mto Wona ulipo mita 300 kutok shuleni hapo na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa,Mawenzi.

Siku mbili baadaye yaani Novemba 12 mwili wa marehemu ulizikwa na Manispaa ya Moshi katika makaburi ya Karanga bila kutolewa kwa muda wa watu ama ndugu kwenda kuutambua mwili huo kama taratibuzinavyotakiwa.

Ndugu wa marehemuwakiongozwa na baba mzazi wa marehemu,Jackson Makundi walibaini kuwa mwili uliozikwa katika makaburi hayo ya karanga ulikuwa wa mpendwa wao na hivyo kuomba kibali cha mahakama ambako Novemba 17 mwaka jana , mahakama ya Hakimu mkazi mjini moshi ilitoa kibali cha kuufukua Mwili huo.

Mwili huo ulifanyiwa uchunguzi wa kitabibu na madaktari katika Hospital ya rufaa ya KCMC na kushuhudiwa na Baba mzazi wa marehemu na katika uchunguzi huo,ikabainika marehemu alikatwa na kitu chenye ncha kali kiunoni,mgongoni,kwenye mapaja na mbavu mbili zilivunjika.

Baba mzazi huyo akawaeleza wanahabari kuwa kulingana na majibu ya uchunguzi huo ni ukweli ulio wazi kuwa,mwanaye aliuawa na kwamba kifo chake kinatia shaka ndipo akavitaka vyombo vya uchunguzi kuwasaka wahusika wa mauaji ya mtoto wake.

Mwili wa marehmu Humphrey ulizikwa desemba 2 mwaka Jana nyumbani kwao katika kijiji cha Komakundi,Moshi Vijijini mazishi ambayo yaliongozwa na Mkuu wa mkoa waKilimanjaro,Anna

Mghwira huku kukiwa hakuna uwakirishi wa viongozi Wa shule hiyo katika shughuli hizo za mazishi.

No comments:

Post a Comment

Popular