Tanzania yapata uwekezaji mkubwa. - KULUNZI FIKRA

Sunday 25 February 2018

Tanzania yapata uwekezaji mkubwa.

 
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe  Charles Mwijage amezindua kiwanda cha Inhemeter ambacho ni cha kwanza nchini kitakachotengeneza mita za Luku.

Waziri Mwijage ameliomba Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kutumia fursa ya kuwepo kwa kiwanda hicho.

“Ninamwomba mwekezaji kuzalisha bidhaa nyingi zenye ubora wa kimataifa na bei nafuu sokoni,” amesisitiza Waziri Mwijage wakati akizindua kiwanda hicho jijini Dar es Salaam.

Amempongeza mwekezaji kwa uamuzi wake wa kuja kuwekeza nchini na kumwahidi kuwa serikali inahamasisha ujenzi na uanzishwaji wa viwanda.

“Wakati umefika wa kuondokana na uchuuzi. Tunataka tuzalishe wenyewe hapa nchini na tuuze nje, simaanishi kuwa hatuhitaji bidhaa za nje hapana zije zile tu zenye ubora stahili,” amesema.

Waziri Mwijage alisema anafuraha kushuhudia uzinduzi wa kiwanda kipya cha 3,307 katika kipindi kifupi. Naye Mshauri Mkuu wa Kiwanda hicho ambaye pia ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhem Meru, alivishauri vitengo vya manunuzi nchini kusaidia ujenzi wa viwanda.

“Hiki ni kiwanda pekee kitakachozaliza mita za Luku nchini. Ni vizuri tukalinda viwanda vyetu vya ndani kwa kuwa wateja wa bidhaa zinazozalishwa hapa kabla ya kukimbilia nje,” alisisitiza.

Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Abraham Rajakili alisema Inhemetre ni kampuni yenye uzoefu wa miaka 20 katika utafiti, uzalishaji na uzambaziji wa mita za Luku.

No comments:

Post a Comment

Popular