Serikali yafikiria kutoa kodi ya utalii kwa watu wote wanaotumia barabara ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. - KULUNZI FIKRA

Thursday 15 February 2018

Serikali yafikiria kutoa kodi ya utalii kwa watu wote wanaotumia barabara ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

 
Serikali inafikiria namna bora ya kubadilisha uelekeo wa eneo la kilometa 50 za barabara ya lami inayopitia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi au kutoza kodi ya Utalii kwa watu wanaotumia barabara hiyo.

Lengo la hatua hiyo ni kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazosababishwa na barabara hiyo kwenye uhifadhi.

Hayo yalisemwa jana mkoani Morogoro na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamisi Kigwangalla kufuatia ombi la uongozi wa Hifadhi hiyo la kuiomba serikali kuchepusha barabara hiyo kutokana na athari mbalimbali za kimazingira, zinazosababishwa na barabara hiyo hasa vifo vya mara kwa mara vya wanyamapori na ukosefu wa mapato ya Serikali.

Awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo mbele ya Waziri Dkt  Kigwangalla, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Gerald Mono alisema licha ya barabara hiyo kuwa na fursa nyingi za kimaendeleo, imekuwa na changamoto nyingi kwenye uendeshaji wa shughuli za uhifadhi.

Alisema wastani wa mnyamapori mmoja hugongwa na gari kila siku katika barabara hiyo, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2014 idadi ya wanyamapori waliogongwa walikuwa 351, mwaka 2015 walikuwa 361 na mwaka 2016 walikuwa 218.

Alisema changamoto nyingine ni uchafuzi wa mazingira, ambapo wastani wa taka ngumu zisizopungua kilo 138. 3 huzalishwa kila siku na watumiaji wa barabara hiyo.

No comments:

Post a Comment

Popular