Serikali kulipa madeni yote ya watumishi. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 8 February 2018

Serikali kulipa madeni yote ya watumishi.

 
SERIKALI imesema wafanyakazi wa serikali na wazabuni wanaoidai watapewa stahiki zao karibuni kwani ipo katika hatua za mwisho za uhakiki wa madeni hayo.

Fedha hizo Sh. bilioni 200 ziliahidiwa na Rais John Magufuli Januari 3, mwaka huu, alipokutana na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Florens Luoga, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Hassan Abbas, aliyasema hayo jana wakati akitoa taarifa ya kila mwezi ya serikali mbele ya waandishi wa habari.

"Tayari fedha zimekabidhiwa Wizara ya Fedha na Mipango, lakini kwa taratibu za serikali lazima uhakiki ufanyike, kwa sasa uko kwenye hatua za mwisho na zitaanza kulipwa wakati wowote," alisema.

Alisema fedha hizo zitalipa watumishi wenye madai ya likizo, safari na mengineyo ambayo yamehakikiwa na pia wazabuni wanaoidai serikali kama ambavyo Rais alisema.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, angeweza kutoa mapema fedha hizo lakini aliona kuna umuhimu wa kuhakiki madeni husika.

"Nina uhakika zitawasaidia wananchi ambao walikuwa waaminifu, waliokuwa wazabuni, zitahakikisha wenye madeni ya ukweli na siyo uongo kupata fedha za kuwasaidia kufanya biashara," alisema Rais Magufuli siku hiyo.

Aidha, alimwagiza Gavana Luoga, kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango ili kwa wanaoidai serikali wenye madeni ya ndani na siyo ya nje na kwamba ni njia ya kukuza uchumi kwa kuwa bilioni 200 zitasambaa kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

Popular