Mwigulu atoa maagizo kwa IGP Sirro kuhusu kifo cha mwanafunzi wa NIT. - KULUNZI FIKRA

Sunday 18 February 2018

Mwigulu atoa maagizo kwa IGP Sirro kuhusu kifo cha mwanafunzi wa NIT.

 
Waziri wa mambo ya ndani Mhe Mwigulu Nchemba amemuagiza Mkuu wa jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro na timu ya uchunguzi kutoka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya kupigwa risasi kwa mwanafunzi Akwilina Maftah.

Waziri Mhe Mwigulu  ametoa maagizo hayo akiwa mkoani Geita wilaya ya Chato wakati wa uzinduzi wa Gereza la wilaya ya Chato.

Waziri Mhe Mwigulu amelitaka jeshi la polisi kuchunguza kwa kina tukio hilo na kuchukua hatua kwa askari aliyehusika na hilo na kuwaambia wananchi nini kinachoendelea.

“Kama Waziri mwenye dhamana nalaani vikali sana tukio la kupoteza maisha ya binti wetu ambaye hakua na hatia, matukio ya namna hii naona yanaanza kujirudia tena kwa kasi matukio ya kupoteza maisha kwa watu wasiokuwa na hatia hasahasa katika masuala yanayohusu siasa ni mambo ambayo hayakubaliki na ninalaani kwa nguvu zote", alisema Mhe Mwigulu.

Pia Mhe Mwigulu amewataka wananchi wote kuepuka vitendo hivi vinavyoweza kusababisha madhara kwa namna moja au nyingine na wanapoona matukio ya namna hii watoe ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili wahusika wafikishwe katika vyombo vya usalama.

No comments:

Post a Comment

Popular