Mrisho Gambo atangaza Neema kwa wakazi wa Arusha. - KULUNZI FIKRA

Thursday 15 February 2018

Mrisho Gambo atangaza Neema kwa wakazi wa Arusha.

 
Mkuu wa Mkoa Arusha, Mrisho Gambo amezindua kamati ya wajumbe tisa ambayo itaanza kupita kwenye sekta binafsi kutoa elimu na kutatua kero sehemu za kazi.

Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo leo Februari 15, 2018 Gambo amesema amewapa hadidu 17 za rejea wajumbe hao kutoka vyombo mbalimbali vya Serikali, ambazo zitawezesha kusaidia kutatua migogoro sehemu za kazi mkoani hapa.

Amesema kamati hiyo ameipa siku 30 kuhakikisha inapita taasisi za sekta binafsi kuzungumza na waajiri na wafanyakazi, ili kuboresha uhusiano kazini.

"Tunataka kamati hii iwe ya kusaidia pande zote siyo ya kuleta migogoro, kama mkikuta kuna matatizo makubwa mnapaswa kutoa elimu na ushauri siyo kukamata watu," amesema.

Amesema miongoni mwa hadidu za rejea ni kuangalia mikataba ya wafanyakazi, ajira zao, usawa wa jinsia, haki za kujiunga na vyama vya wafanyakazi na uwasilishwaji michango katika mifuko ya hifadhi ya jamii.

Mjumbe wa kamati hiyo, Froviana Chacha kutoka Idara ya Kazi mkoa Arusha amesema wanatarajia watapunguza migogoro kazini.

"Tumekuwa tukipokea malalamiko mengi ya wafanyakazi na baadhi yanatokana na uelewa mdogo wa sheria kwa waajiri na waajiriwa, hivyo tutatumia kamati hii kutoa elimu" amesema.

Naye mjumbe mwingine kutoka Mamlaka ya Usalama Sehemu za Kazi (Osha), Elizabeth Mtire amesema kuna tatizo la kutofuatwa sheria sehemu za kazi hivyo wataelimisha.

No comments:

Post a Comment

Popular