Mkuu wa wilaya atoa onyo Kali kwa wafanyabiashara. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 8 February 2018

Mkuu wa wilaya atoa onyo Kali kwa wafanyabiashara.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam, Sophia Mjema amezuia upangaji wa biashara barabara za mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) mtaa wa Kongo na kuwataka wafanyabiashara kupanga biashara zao katika maeneo manne yaliyotengwa huko.

Pia amepiga marufuku uwekaji wa majiko unaofanywa na wafanyabiashara wa chakula kwa kuwa majiko hayo yanatajwa kuharibu miundombinu ya barabara wanamofanyia. Mjema alipiga marufuku hiyo alipokuwa akitembelea miradi ya barabara tano na jengo la ofisi za mradi huo jana inayotekelezwa katika Manispaa hiyo yenye lengo la kupunguza msongamano katika maeneo mbalimbali ya Jiji.

Barabara hizo ni Kongo, Olympio, Kiungani, Mmbaruku na jengo la ofisi za mradi huo zenye thamani ya Sh bilioni 11 ambazo zinatarajiwa kukabidhiwa katika manispaa hiyo Februari 27.

Alisema upangaji wa bidhaa katika barabara unachangia misongamano mkubwa wa watu na magari kwani biashara nyingi zimewekwa katika barabara za waenda kwa miguu. “Barabara hizi bado hatujakabidhiwa lakini changamoto hii ya upangaji wa bidhaa hizi ni kubwa.

Niwasihi wafanyabiashara mitaa ya kufanya biashara tayari tumeitenga, mwende huko mkafanye biashara zenu na wenye fremu mhakikishe mnaweka ndani ya fremu zenu bila kuingia katika maeneo ya barabara,” alisema.

Akizungumzia jengo hilo la ofisi, alisema litakuwa na maabara ambayo itatumika kupima kokoto, mchanga na udongo utakaokuwa unatumika kujenga barabara ili ziwe imara. “Hatutaki baada ya muda barabara zinakuwa na mashimo kwa hiyo maabara hii itakuwa inafanya kazi kubwa kuhakikisha tuna barabara bora zenye uhai mrefu,” aliongeza Mjema.

Msimamizi wa Mradi huo, Elius Rwegasira alisema mradi huo ulikumbwa na changamoto za miundombinu ya umeme, simu na maji. Alisema miundombinu hiyo haikuwa vizuri lakini kupitia mradi huo wameangalia yote na kuhakikisha iko sawa na mifumo kuboreshwa kuwa rahisi kwa maboresho ya baadaye kwa kuwa miundombinu mingi imepitishwa chini.

No comments:

Post a Comment

Popular