Mbunge afunguka mazito kuhusu waziri wa Elimu. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 8 February 2018

Mbunge afunguka mazito kuhusu waziri wa Elimu.

 
Mbunge wa Ulanga (CCM) Mhe  Goodluck Mlinga amefunguka na kumchana Waziri wa Elimu, Profesa. Joyce Ndalichako na kusema kuwa hafai kuendelea kushika nafasi hiyo kutokana na ukweli kwamba sekta ya elimu imezidi kushuka zaidi na wanafunzi kufeli.

Mhe Mlinga amesema hayo Bungeni na kudai kuwa shule za Serikali zimezidi kufanya vibaya katika mitihani ya Taifa huku shule za watu binafsi zikionyesha kufanya vyema zaidi na kudai bila shule binafsi Waziri Ndalichako angekuwa Waziri wa Masifuri.

"Suala langu la kwanza ni ushukaji wa elimu kwa shule za Serikali za Tanzania, kwa muda wa miaka miwili sasa Waziri wa Elimu amedumu katika wizara hii lakini tumeshuhudia uangukaji mkubwa wa shule za sekondari za serikali hivyo Mhe  Ndalichako anaweza kujipima mwenyewe kwa kiasi gani ni mzuri na kiasi gani ni mbaya na hii inanipa hofu sijui Maprofesa wa Tanzania wanatatizo gani? Ushauri wangu mimi kwa Rais angechaguliwa mtu kama Msukuma au Lusinde ambao wameishia darasa la saba kuwa Mawaziri wa Elimu kwa sababu wanajua matatizo gani mpaka wakashindwa kusoma. Maprofesa wa Tanzania wanaongoza kutoa miongozi matokeo yake elimu inafeli" alisema Mhe Mlinga.

Mhe Mlinga aliendelea kutoa yake ya moyoni kuwa, "Mwaka huu matokeo ya shule za sekondari za serikali katika shule bora 10 hakuna na sisi tulizoeaga kusikia Mzumbe, Kilakara lakini saizi hazipo na katika shule 100 bora za sekondari shule za serikali zipo nne tu jamanii hii si aibu, Waziri wa Elimu una kitu gani cha kutuambia sasa maana umeonyesha kufeli halafu ukija unawapiga vita watu wenye shule binafsi, sasa kwa mfano hizi shule za binafsi tungeziondoa kwenye orodha ya zile shule 100 bora wewe si ungekuwa Waziri wa masifuri? Ehh angekuwa waziri wa masifuri maana shule za sekondari za serikali zote zimefeli" alisisitiza  Mhe Mlinga.

Mbali na hilo  Mhe Mlinga aliweka wazi kuwa shule za sekondari ya serikali zinapata matokeo mabovu kutokana na mazingira mabovu ya shule zenyewe kuanzia kwa walimu kwani walimu hao muda mrefu wanaidai serikali malipo yao na wamekuwa hawalipwi kwa kigezo cha serikali kusema wanahakiki, lakini pia amedai walimu wanapangiwa vijijini sehemu ambazo hazina miundombinu mizuri.

No comments:

Post a Comment

Popular