Mbowe ataka Jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kifo cha kiongozi wa chadema. - KULUNZI FIKRA

Tuesday 13 February 2018

Mbowe ataka Jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kifo cha kiongozi wa chadema.

 
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mhe Freeman Mbowe amesema kiongozi wa chama hicho katika Kata ya Hananasif, Daniel John amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.

Mhe Mbowe akizungumza na waandishi wa habari Jana  Februari 13,2018 amesema John alitoweka siku moja iliyopita.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema hana taarifa hizo lakini anawasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni.

Amesema baada ya mawasiliano atatoa ufafanuzi kesho Februari 14,2018. Mbowe amesema John ambaye ni katibu kata alitoweka akiwa na Reginald Mallya ambaye alijikuta yupo ufukweni mwa bahari.

Mhe Mbowe amesema walitoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa John na kwamba, walipokwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) walielezwa kuna mwili ulipelekwa na polisi.

Amesema mwili huo ulitambuliwa na mkewe John na una michubuko inayoashiria alikabwa, una jeraha la panga kichwani na upande mmoja wa kichwa umebonyea kuashiria alipigwa na kitu kizito.

Kuhusu Mallya amesema alipigwa panga kichwani na alivunjwa mkono. Mbowe ametaka polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Mallya aliyekuwapo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari amesema walikuwa wakitembea na John ndipo waliposimamishwa na kuingizwa ndani ya gari.

Amedai alipigwa hadi kupoteza fahamu na alipozinduka alijikuta ufukweni alikojikokota hadi barabarani ambako alipata msaada wa bajaji na alikwenda Hospitali ya Mwananyamala alikotakiwa kuwa na taarifa ya Polisi ambayo aliipata Kituo cha Polisi Oysterbay.

No comments:

Post a Comment

Popular