Jeshi la polisi limewachia viongozi wa chadema kwa dhamana. - KULUNZI FIKRA

Tuesday 20 February 2018

Jeshi la polisi limewachia viongozi wa chadema kwa dhamana.

 
Viongozi watano wa Chadema kati ya saba waliokwenda Kituo Kikuu cha Polisi kuitikia wito wa kamanda  wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, wameachiwa kwa dhamana.

Walifika kituoni hapo Leo Februari 20, 2018 saa 6: 10 mchana na kuachiwa saa 7:45 mchana.

Viongozi walioitwa na  Kamanda Mambosasa ni mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mhe Freeman Mbowe, katibu mkuu wa chama hicho, Dkt Vincent Mashinji, naibu makatibu wakuu John Mnyika (bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Pia wamo, mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Mhe  Halima Mdee; mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, Mhe  John Heche na  Mhe Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.

Waliofika leo kituoni hapo na kuachiwa ni  Mhe  Ester Bulaya, Mhe Halima  Mdee, Mhe Esther  Matiko, Mhe John Heche na  Mhe John Mnyika.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mhe Mnyika amesema kupitia wakili wao, Peter Kibatala  wamepewa dhamana na kutakiwa kuripoti tena kituoni hapo, Februari 27, 2018.

Amedai kuwa fununu zilizopo ni kwamba wanaweza kufunguliwa shataka la kuandamana bila kuwa na kibali.

"Tumefika hapa lakini hatujahojiwa hivyo tumepewa dhamana na tutaripoti siku ya Jumanne wiki ijayo,” amesema Mhe Mnyika

Wito wa viongozi hao polisi umekuja siku siku nne tangu kutokea kwa kifo cha Akwilina Akwiline, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usfairishaji (NIT).

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 16, 2018 akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.

No comments:

Post a Comment

Popular