Hospitali ya Bugando yahujumiwa na watumishi Wake. - KULUNZI FIKRA

Tuesday 20 February 2018

Hospitali ya Bugando yahujumiwa na watumishi Wake.

 
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) jijini Mwanza, Dkt Abel Makubi, amesema kuna baadhi ya watumishi wamekuwa wakiihujumu hospitali hiyo kwa kuhamishia wagonjwa kwenye hospitali na vituo binafsi vya afya.

Amekiri kuwepo matukio ya uvunjifu wa amani kwa watumishi wa hospitali hiyo ya Kanda ya Ziwa, lakini pia kauli chafu na dhihaka kwa baadhi ya wagonjwa na ndugu wanaowasindikiza hospitalini hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya hospitali hiyo Jana alisema, baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo kwa kushirikiana na watu au mawakala wao (vishoka) huwalaghai wagonjwa na kuwahamishia vituo binafsi vyenye uwezo mdogo katika huduma za matibabu.

Ametoa mfano wa tukio la hivi karibuni la mgonjwa aliyerubuniwa na kukubali kuhamishiwa kituo binafsi ambako hata hivyo alifariki dunia baada ya kukosa matibabu stahiki.

Dkt  Makubi ametoa mwito kwa wananchi kuwa makini na kujihadhari na walaghai hao ikiwa ni pamoja na kuwaripoti kwa viongozi wa hospitali hiyo, kupitia namba za simu zilizobandikwa kwenye maeneo mbalimbali ya kutolea huduma.

Kuhusu uvunjifu wa amani, alitaja tukio la Februari 18, mwaka huu, ambapo watu kadhaa walimshambulia kwa kipigo muuguzi wa zamu hospitalini hapo, baada ya kupewa taarifa za kifo cha ndugu yao aliyekuwa amelazwa akitibiwa maradhi ya numonia na shinikizo la damu.

"Walimshambulia muuguzi huyo kwa madai ya uzembe, lakini pia waliwashambulia na kuwajeruhi walinzi watatu wa hospitali waliokuwa wamewazuia kulala katika wodi alikokuwa amelazwa mgonjwa wao," alisema Dkt Makubi.

No comments:

Post a Comment

Popular