Hoja ya Zitto kabwe ya maridhiano ya kitaifa yawaibuwa Wasomi. - KULUNZI FIKRA

Sunday 25 February 2018

Hoja ya Zitto kabwe ya maridhiano ya kitaifa yawaibuwa Wasomi.

Hoja ya kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe kuhusu mkutano wa kitaifa wa maridhiano imeungwa mkono na wadau wakisema ina tija kutokana na matukio yanayojitokeza nchini.

Hoja ya Zitto ni sawa na iliyotolewa Februari 22 katika mkutano wa viongozi wa dini na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) uliopendekeza kuonana na Rais John Magufuli ili kujadiliana naye masuala yanayoendelea nchini.

Juzi, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha alisema changamoto za kisiasa zinapaswa kujadiliwa na kukubaliwa kwa mujibu wa kanuni za demokrasia ya vyama vingi.

Mbunge huyo alishauri wahusika wawe ni viongozi wa vyama vya wafanyakazi, vyama vya wafanyabiashara, wakulima na wafugaji.

Zitto alisema hali ya kisiasa sasa si ya kuwaachia wanasiasa pekee kwa kuwa inahusu uhai wa watu wengine ambao hata hawajihusishi na siasa.

Hoja ya kuwapo majadiliano inatokana na kile kinachoelezwa ni kuibuka kwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwamo utekaji na mauaji.

Baadhi ya matukio hayo ni yale ya hivi karibuni ya kuuawa kwa diwani wa Namwawala wilayani Kilombero mkoani Morogoro, Godfrey Luena Februari 22 akiwa nyumbani kwake. Diwani huyo anatarajiwa kuzikwa leo.

Tukio lingine ni la kiongozi wa Chadema Kata ya Hananasif jijini Dar es Salaam, Daniel John ambaye aliuawa na mwili wake kuokotwa ufukweni Coco na la kupigwa risasi aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini Februari 16.

Alipotakiwa kutoa maoni yake jana, katibu mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Magembe Makoye alisema jamii ya wafugaji ni miongoni mwa makundi yanayokabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji majadiliano.

“Ni wazo zuri kutafuta muafaka, kama kuna watu wanafanya hivyo sisi tunawaunga mkono,” alisema.

Makoye aliungwa mkono na mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga ambaye alisema anaunga mkono jitihada zozote za kutafuta utulivu hasa ikizingatiwa kwamba kuna matukio ya umwagaji damu ambayo yamejitokeza katika siku za hivi karibuni.

“Matukio ya hivi karibuni yanaharibu utulivu na amani ya nchi, mfano mauaji ya binti Akwilina, diwani wa Chadema (Kata ya Namwawala-Godfrey Luena) kukatwa mapanga, haya ni matukio mabaya na ndiyo maana tutaunga mkono,” alisema Makunga.

Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema hoja ya Zitto haina tofauti na moja ya maazimio ya kikao cha viongozi wa dini na Kituo cha Demokrasia ya kuitishwa kikao maalumu cha majadiliano.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza aliunga mkono hoja ya mkutano wa kutafuta muafaka akisema, “Watawala wanaogopa watawaliwa, watawaliwa wanaogopa watawala, polisi wanaogopa waandamanaji, waandamanaji wanaogopa polisi.

Hata hivyo, Askofu William Malanga, mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maaskofu na masheikh ya maadili, amani na haki za binadamu kwa jamii ya madhehebu yote Tanzania alisema kabla ya kufanyika kikao cha maridhiano lazima kujua wanakwenda kuridhiana na nani.

“Suala si maridhiano, tunapaswa kujiuliza tunaridhiana na nani, wanaoharibu amani ya nchi wanajulikana? Tunakwenda kuridhiana na mtu ambaye hajulikani? Bila kujua tunaridhiana na nani hilo kongamano haliwezi kufanikiwa,” alisema Askofu Malanga.

Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya alisema, “Kila kitu ukiona kinaanza kumea kinabidi kidhibitiwe mapema, mambo ya kudhalilisha wafanyakazi hayakuwepo awali, tuna sheria na taratibu zake za kumshughulikia mfanyakazi anapokosea.”

No comments:

Post a Comment

Popular