Askari polisi afariki dunia kwa kujirusha kutoka kwenye gari. - KULUNZI FIKRA

Wednesday 28 February 2018

Askari polisi afariki dunia kwa kujirusha kutoka kwenye gari.

 
Sajenti Bernard Mkulula (50) wa Kituo cha Polisi Magumu wilyani Serengeti, Mara amefariki dunia baada ya kujirusha kupitia dirishani na kukanyagwa alipokuwa kwenye gari akiwapeleka mahabusu mahakamani.

Tukio hilo lililozua gumzo mjini Magumu lilitokea saa 3:30 asubuhi wakati askari huyo akiwa katika lori aina ya Leyland na mahabusu.

Baada ya tukio hilo, mmoja wa askari wenzake ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe kwa kuwa si msemaji, alisema Mkulula alikuwa akilalamikia masuala kadhaa ya kifamilia.

"Wakati tuko njiani kwenda mahakamani alijiapiza kuwa leo lazima afe; kweli amefariki kwa kujiua kwa kujirusha kwenye tairi la gari la Polisi", alisema askari huyo ambaye alishuhudia tukio hilo.

"Baada ya kuruka kutoka kwenye gari, alining'inia akiwa ameshikilia kioo kidogo cha pembeni kabla ya kuangukia kwenye tairi na gari kupita likamvunja miguu yote miwili hadi eneo la nyonga".

Katibu wa Hospitali Teule ya Nyerere, Mbona Kazare alisema askari huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu. Alisema alifikishwa hospitalini hapo akiwa mahututi.

"Alikuwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili, alivunjika miguu; taarifa kamili ya chanzo cha kifo zitatolewa na daktari", alisema Kazare.

Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu ambaye ni kati ya watu waliofika hospitali ya Nyerere kufuatilia suala hilo, aliwataka askari na wananchi kutumia njia sahihi ikiwemo majadiliano au hatua za kisheria kutatua changamoto zinaziwakabili.

"Ni simanzi na huzuni kubwa kwa mtu, tena askari polisi kujiua kwa kujirusha kwenye tairi ya gari linalotembea, mtu akiwa na tatizo ni vyema kushirikisha wenzake au uongozi kwa ajili ya ufumbuzi", alisema Babu.

No comments:

Post a Comment

Popular