Tume ya Uchaguzi yatoa maamuzi mazito kwa mgombea ubunge jimbo la Kinondoni. - KULUNZI FIKRA

Saturday, 27 January 2018

Tume ya Uchaguzi yatoa maamuzi mazito kwa mgombea ubunge jimbo la Kinondoni.

 
Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) yakubaliana na maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo ya kuruhusu mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Salum Mwalim kuendelea kuwa mgombea wa ubunge Jimbo la Kinondoni.

Maamuzi hayo yalifikiwa katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika tarehe 26 Januari 2018 siku ya Ijumaa, baada ya tume kupitia rufaa hizo na kuamua mgombea huyo wa CHADEMA kuendelea na uchaguzi.

Mgombea Ubunge Jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya CUF alipinga maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo kuhusu pingamizi alilomuwekea Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Aidha, kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 44 (5) cha sheria ya uchaguzi ya serikali za mitaa, sura ya 292, ikisomwa pamoja na Kanuni za 28 na 29 za Kanuni za serikali za mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015.

Tume ilipokea Rufaa tano (5) za wagombea  udiwani  kutoka katika Kata ya Isamilo – Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wakipinga Maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo.  Rufaa tatu (3) ni za wagombea walioondolewa kwenye kugombea ili warejeshwe na Rufaa mbili (2) zinaomba Tume itengue uteuzi wa mgombea Udiwani aliyeteuliwa katika Kata hiyo.

“Kuhusu Rufaa za Wagombea Udiwani Kata ya Isamilo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, kupinga kuondolewa kugombea Udiwani katika Kata hiyo, Tume imewarejesha kuwa Wagombea Udiwani wawili wa vyama vya CHADEMA na CUF,” ilifafanua  taarifa ya NEC.

Tume pia imekubaliana na maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi ya kumuondoa katika orodha ya wagombea Udiwani mgombea wa chama cha UDP. Hivyo hatakuwa mgombea katika kata hiyo

Wakati huo huo tume imekataa rufaa mbili zilizokuwa zinapinga uteuzi wa mgombea wa CCM aliyeteuliwa katika Kata hiyo na hivyo, mgombea wa CCM anaendelea kugombea Udiwani katika kata husika.

No comments:

Post a Comment

Popular