Taharuki kwa Wateja wa benki baada ya BOT kuzifunga benki tano. - KULUNZI FIKRA

Friday, 5 January 2018

Taharuki kwa Wateja wa benki baada ya BOT kuzifunga benki tano.

TAHARUKI imejitokeza katika maeneo mbalimbali nchini baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuzifungia benki tano kuendesha shughuli zake hapa nchini baada ya kubainika kufi lisika.

Jana Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alizitaja benki zilizofungwa kuwa ni Covenant Bank for Women (Tanzania) Limited, Efatha Bank Limited, Njombe Community Bank Limited, Kagera Farmers’ Co-operative Bank Limited na Meru Community Bank Limited. Profesa Ndulu alisema kuwa BoT itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika benki kwa lengo la kuleta uhimilivu katika sekta ya fedha nchini.

Alisema katika kuhakikisha usalama wa fedha za wateja wa benki hizo, BoT imeiteua Bodi ya Bima ya Amana kuwa Mfilisi wa benki hizo tano na kuwataka wateja wanaotumia huduma za benki hizo kuwa wavumilivu kwa sasa.

Akizungumzia hatua za kuzifungia benki hizo za wananchi, Profesa Ndulu alisema, mwaka 2012, Benki Kuu iliongeza kiwango cha chini cha mtaji wa benki za wananchi, Community Banks, kuwa Sh bilioni mbili. Alisema, benki hizo pia zilipewa muda wa miaka mitano kuhakikisha kuwa zinaongeza mtaji kufikia kiwango kipya, muda ulioisha Juni 2017.

Alisema hata hivyo muda uliongezwa tena kwa kipindi cha miezi sita hadi kufikia Desemba 31, mwaka jana ambapo bado benki nane hazikuweza kuongeza mtaji kufikia kiwango kamili kilichohitajika.

Alisema lakini ni benki tano kati ya hizo nane zenyewe zilishindwa kuandaa na kuwasilisha Benki Kuu mpango mkakati unaokubalika wa kuongeza mtaji ambao ungezifanya kuwa benki endelevu.

Alisema kuwa kutokana na kushindwa kukidhi Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, BoT imeamua kuzifunga, kusitisha shughuli zake zote za kibenki, kufuta leseni zake za biashara ya kibenki pamoja na kuziweka chini ya ufilisi benki hizo tano kuanzia hiyo jana. BoT imeiteua Benki ya Amana kuwa mfilisi wa benki hizo tano.

“Lakini zile benki tatu kati ya hizo tano ambazo licha ya kuwa na kiwango kisichokidhi matakwa ya kisheria, zenyewe zimewasilisha Benki Kuu mpango mkakati unaokubalika wa kuongeza mtaji na kuzifanya ziwe endelevu hivyo zimepewa muda wa miezi sita hadi Juni 30 mwakani.

“Ndani ya miezi hiyo sita ziwe zimeshaweka mtaji na kutekeleza mipango hiyo inayotakiwa na endapo zitashindwa kutekeleza agizo husika kufikia hiyo Juni 30, mwakani basi BoT itazifutia leseni, kusimamisha shughuli zake benki hizo na kuziweka chini ya ufilisi,” alisema Profesa Ndulu.

Alizitaja benki hizo kuwa ni pamoja na Kilimanjaro Co-operative Bank Limited, ambapo Profesa Ndulu alisema kuwa mmiliki wa benki hiyo ambaye ni Chama cha Ushirika mkoani Kilimanjaro, KNCU, amekubali kuongeza mtaji kutokana na mapato yatakayotokana na uuzwaji wa baadhi ya mali zake na michango kutoka vyama mbalimbali ambavyo ni wamiliki wa benki.

Nyingine ni Benki ya Wanawake Tanzania ambapo Profesa Ndulu alisema kuwa mmiliki wa benki hiyo ambaye ni serikali imeshakaribisha taasisi mbalimbali za umma kuwekeza kwenye mtaji wa benki hiyo. Pia Benki ya NMB, kwa upande wake imeshaonesha nia ya kuwekeza kwenye benki hiyo na kuifanya kuwa dirisha la kuwasaidia wajasiriamali wanawake.

Alimalizia kwa kuitaja Tandahimba Community Bank Limited, ambapo kwa sasa ipo kwenye ushirikiano na Benki ya CRDB katika mkataba wa miaka mitatu tangu mwaka 2015, ambapo CRDB inaisaidia benki hiyo katika nyanja za uongozi na ukwasi ambapo faida imeanza kuonekana. Taharuki kwa wateja Kutokana na kufungiwa kwa benki hizo, wananchi mbalimbali jana walizungumza na gazeti hili na kueleza namna hatua hivyo ilivyowashitua na kuleta taharuki kwao binafsi na familia zao.

Mteja wa Benki ya Efatha, ambaye ni mkazi wa Mwenge, Dar es Salaam, Emmanuel Msangi alisema kuwa amekuwa akiweka fedha zake kwenye Benki ya Efatha akihudumiwa kwenye tawi la Mwenge yalipo Makao Makuu yake na alipofika jana alishituka kukuta imefungiwa. Alisema, alikwenda katika tawi hilo ili kuchukua fedha kwa ajili ya kumalizia ada ya shule ya mwanaye lakini alijikuta akishindwa kufanya hivyo, kutokana na matangazo ya BoT aliyoyakuta hapo kuonesha benki hiyo kufungiwa.

“Najua huwa kunakuwa na muda wa siku kadhaa baada ya kuzifunga hizo benki kabla ya kuruhusiwa kutoa fedha sasa ni sijui nitawezaje kumalizia ada na kuendelea na shughuli nyingine ili hali fedha zipo humo,” alisema Msangi. Akizungumza kwa simu na gazeti hili, mkazi wa Bukoba mkoani Kagera, Nana Lutahingwa alisema ameshtushwa na kufungiwa kwa Benki ya Kagera Farmers’ Co-operative kwa kuwa alikuwa akiitumia kuweka fedha na wanachama wenzake wa umoja wa wakulima.

Viongozi Njocoba kuburuzwa kortini Kufuatia BoT kuifutia leseni na kuifungia benki ya wananchi Njombe (NJOCOBA) taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Njombe (Takukuru) imesema inachunguza mwenendo na taratibu za utoaji mikopo katika benki hiyo na wakisha kamilisha watawafikisha mahakamani viongozi hao na wote watakao bainika na ubadhirifu katika benki hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Njombe, Charles Shamsulla alisema katika uchunguzi wao wa awali wamebaini kuwa watendaji wa benki hiyo wakiwemo wakurugenzi wa Bodi walikuwa wakikiuka taratibu za kibenki za utoaji mikopo kwa baadhi ya wateja. Alisema walikuwa wakitoa mikopo kwa baadhi ya wateja kwa kutumia dhamana za kughushi, kutoa mikopo mikubwa kuliko dhamana walizoweka kwa mujibu wa sheria na matokeo yake mikopo kushindwa kulipika.

“Kutokana na hali hiyo, Njocoba hadi kufikia mwaka wa fedha 2016/2017 iliweza kupata hasara ya jumla ya shilingili 848,808,771 ambapo kutokana na hasara hiyo benki imejikuta ikishindwa kujiendesha na kushindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi,” alisema Shamsulla. Alisema baadhi ya wateja waliruhusiwa kuchukua mikopo zaidi ya mmoja bila ya kufuata taratibu na kubadilisha majina ili hali ni walewale.

“Kwa mfano mtu anachukua leo kama mkopo binafsi na kesho yake mtu huyo huyo anakuja kama kampuni kuchukua mkopo mwingine kabla hajamaliza mkopo wa kwanza,” alisema Shamsulla. Aidha aliongeza kuwa baada ya uchunguzi huo kukamilika watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa wahusika, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani kujibu mashtaka ya jinai kwa vitendo vya rushwa na kuisababishia hasara benki ya wananchi njombe. Wakati huo huo, jana baadhi ya wateja wa Benki ya Njocoba waliohojiwa walionesha kushikwa na butwaa.

Mwandishi wa habari hizo alitembelea katika benki hiyo iliyopo katikati ya mji Wa Njombe, na kushuhudia wateja waliofika kwenye benki hiyo, wakikutana na matangazo yaliyobandikwa nje ya lango kuu la kuingia kwenye benki hiyo. Baadhi ya wateja waliohojiwa walilalamikia kushindwa kuchukua fedha walizokuwa wameweka kwenye akaunti zao na kudai kuwa kufuatia hatua hiyo hali zao kimaisha zitakuwa ngumu hasa ikizingatiwa kuwa huu ni msimu wa kupeleka watoto shule.

“Hili suala mimi binafsi limeniathiri kwa kiasi kikubwa, kwa sababu nilitegemea kuja kuchukua pesa hapa benki, lakini nimekuta wamefunga na sijui hatma yake nini,” alisema Peter Mligo. Wateja Benki ya Meru wafurika tawini Katika hatua nyingine wateja waliokuwa na akaunti katika Benki ya Meru Community iliyopo eneo la Usa River wilayani Arumeru mkoani Arusha walifurika katika benki hiyo kujua hatima ya fedha zao.

Majira ya saa nne asubuhi jana wateja hao ambao pia ni pamoja na Vikundi vya Akiba na Mikopo (Vikoba) walionekana kurandaranda nje ya eneo hilo la benki wakitaka kujua hatma ya fedha zao huku wengi wa wanawake wa vikundi hivyo wakiangua vilio kwenye lango kuu la benki hiyo. Licha ya wateja hao pia wapo watu binafsi na taasisi za dini na za binafsi ambazo zilikuwa zimenunua hisa katika benki hiyo ambayo asilimia kubwa ya wananchi wa Wilaya ya Arumeru wamekuwa wakiitumia benki hiyo katika shughuli mbalimbali za huduma za fedha.

Kundi lilingine lililopatwa na kiwewe ni pamoja na madereva bodaboda ambao wengi wao walikuwa wateja wakubwa wa benki hiyo ambao nao walionekana kufurika katika eneo hilo pamoja na wajasiriamali wadogo wadogo idadi kubwa ikiwa ni wanawake. Wakizungumza kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini viongozi wa vikundi mbalimbali wa Vikoba walionekana nje ya banki hiyo wakitaka kuoanana na uongozi lakini waligonga mwamba kutokana na ulinzi mkali wa polisi uliokuwa umeimarishwa eneo hilo la benki.

Kwa upande Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Elishilia Kaaya alisema benki hiyo imefungwa kutokana na kutofikia matakwa ya BoT ya kuwataka wawe na mtaji wa Sh bilioni 2. “Tumeumia sana kwa benki yetu kufungwa. Niwatoe hofu tu kuwa benki yetu si kwamba imefilisika ni mtaji wetu mdogo kutokana wateja wetu vipato vyao kuwa ni vya kawaida.”

No comments:

Post a Comment

Popular