Rais Magufuli atoa maagizo mazito kwa mabalozi. - KULUNZI FIKRA

Saturday, 20 January 2018

Rais Magufuli atoa maagizo mazito kwa mabalozi.

Amesema ni vyema mabalozi hao wakawa wanaandika walichoifanyia nchi kila baada ya robo ya mwaka ili wale watakaoonekana hawajafanya lolote atengue tuezi zao.

Alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na wafanyakazi wa wizara hiyo kwenye ukumbi wa Julius Nyerere.

"Waziri (Mahiga) kuanzia leo waandikie barua kila mmoja awe anatoa ripoti ili tukiona kuna balozi yoyote yuko kule na hajafanya lolote nitengue uteuzi wake," alisema Rais Magufuli ambaye alibainisha balozi kama huyo "atabaki na jina la balozi lakini siyo balozi".

"Wizara hii ni muhimu sana kwenye mambo ya nchi hii, mambo ya mahusiano, mambo ya uchumi hii wizara ni muhimu. Inawezekana hatujachelewa, tubadilike na tufanyekazi."

Rais Magufuli alisema zaidi: "Wakupe taarifa kila baada ya robo mwaka na Balozi ambaye atakuwa hakusanyi mapato vizuri na kuinua biashara na uwekezaji, atakuwa hafai kuendelea kuwa Balozi. Tena kawaambie kabisa kwenye suala hili hakuna mchezo."

Aidha, Rais Magufuli alimtaka Waziri Mahiga na watendaji wa wizara yake kufuatilia kwa ukaribu na kushirikiana na Mawaziri wanaohusika katika utekelezaji wa mikataba mbalimbali ambayo Tanzania imetiliana saini na nchi mbalimbali duniani.

Rais Magufuli alisema hataki kusikia utekelezaji wa mikataba ambayo baadhi yake inahusisha miradi mikubwa yenye manufaa kwa nchi ikikwama ama kusuasua.

"Mnapokuwa mnahitaji taarifa kutoka wizara nyingine kama ni Waziri muandikie Waziri mwenzako, kama ni Katibu Mkuu muandikie Katibu Mkuu mwenzako, halafu nakala ya barua ilete kwangu kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi. Nataka nione huyo atakayechelewesha ama kutotoa taarifa."

Kuhusu usajili wa meli, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar Balozi Ali Abeid Karume kusitisha usajili wa meli mpya hapa nchini mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.

Aalisema mpaka sasa kuna meli 470 ambazo zimepewa vibali hivyo na aliagiza zikaguliwe zote na vyombo vyote vya dola na zile zinazoonekana zina mwelekeo huo huo wa kubeba vilipuzi na dawa za kulevya zifutiwe leseni.

"Mawaziri husika nimezungumza nao na wamenifafanulia kwa hiyo katika maaagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais (juzi) nimeongeza mengine maana haiwezekani nchi yetu kila siku inachafuliwa," alisema Rais Magufuli.

Jumla ya meli tano zinazopeperusha bendera ya Tanzania zimekamatwa sehemu mbalimbali duniani kwa makosa ya kiuhalifu katika kipindi kifupi kilichopita.

Alisema watu hao wenye kusafirisha vilipuzi na dawa za kulevya hupenda kutumia meli chakavu kusafirisha vitu vyao zikiwa na bendera ya Tanzania ili hata kama watashtukiwa na zitakamatwa wasipate hasara.

"Maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais (Alhamisi) yaendeleee lakini nimeongeza mengine (na) kuanzia leo hakuna kutoa usajili kwa meli yoyote ya kutoka nje; iwe Tanzania Bara au Tanzania Visiwani mpaka suala hili lipatiwe ufumbuzi na timu tuliyounda ikamilishe kazi yake," alisema Rais Magufuli.

"Lakini pia baada ya kazi kukamilika utaratibu wa kutoa leseni kwa meli zinazotaka kutumia bendera yetu uratibiwe na pande zote za muungano na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vihusike.

No comments:

Post a Comment

Popular