Mvua yasababisha maafa makubwa mkoani Dodoma. - KULUNZI FIKRA

Saturday, 6 January 2018

Mvua yasababisha maafa makubwa mkoani Dodoma.

Katika tukio mojawapo litokanalo na athari za mvua hiyo, watu wawili wanahofiwa kufariki dunia katika eneo la kata ya Kikombo, Manispaa ya Dodoma baada ya gari lao kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha juzi na kuharibu madaraja matatu.

Taarifa ya hofu ya vifo vya watu hao ilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkao wa Dodoma, Gilles Muroto, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt Binilith Mahenge, alitembelea eneo hilo na kuelezwa kuwa madaraja matatu ndiyo yaliyosombwa na mvua na kwamba, mojawapo ndilo lililohusika katika tukio la gari kusombwa na watu wawili kudhaniwa kuwa wamefariki dunia.

Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads), mkoa wa Dodoma, Leonard Chimagu, alimueleza Mkuu wa Mkoa huo, Dkt Binilith Mahenge kuwa mbali na hofu ya vifo, pia madaraja hayo yaliyosombwa yamesababisha kukatika kwa mawasiliano ya barabara.

“Mpaka hivi sasa jumla ya madaraja matatu yameharibiwa na mvua, Kikombo mawili na Hombolo moja… niwaombe wananchi wachukue tahadhari hasa katika kipindi hiki cha mvua kwa sababu madaraja mengi yameharibika,” alisema Chimagu mbele ya wananchi waliokuwapo wakati wa ziara hiyo ya Dkt Mahenge.

Katika tukio lingine, Dkt Mahenge aliamuru kufungwa na pia akapiga marufuku shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu zilizokuwa zinafanyika katika eneo la machimbo ya Nzuguni, Manispaa ya Dodoma baada ya mtu mmoja kufariki kwa maji wakati akiwa ndani ya shimo.

Aidha amemwagiza Kamishna wa Madini Kanda ya Kati kushirikiana na uongozi wa Manispaa na Jeshi la Polisi kufukia mashimo yote ambayo yalikuwa yanatumika kwa jili ya uchimbaji wa madini hayo.

Dkt Mahenge alitoa agizo hilo jana wakati alipotembelea machimbo hayo baada ya kutolewa kwa taarifa ya mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Ramadhani Haruna kufariki duni akiwa katika shughuli za uchimbaji wa madini hayo.

Dkt  Mahenge pia alitoa ubani wa Sh. 100,000 kwa familia mbili zilizokumbwa na msiba, ikiwamo pia ya David Luinga aliyekufa kwa kutumbukia katika karo lililojaa maji ya mvua pamoja na ile ya Haruna aliyekufa kwenye shimo wakati akichimba madini.

Kamanda Muroto, aliwataka watu wote kutii amri iliyotolewa ya kutojihusisha na shughuli za uchimbaji eneo hilo na kwamba, yeyote atakayekiuka atachukuliwa hatua kali za kisheria

No comments:

Post a Comment

Popular