Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kuigonga ndege ya Fastjet. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 18 January 2018

Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kuigonga ndege ya Fastjet.

 
Mkazi mmoja wa mkoa wa Mwanza amefariki dunia baada ya kuigonga ndege ya FastJet iliyokuwa ikiruka katika uwanja wa ndege wa Mwanza kuelekea Dar es salaam.

Akizungumza na kulunzifikra blog leo Januari 18, 2018 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela amesema tukio hilo la aina yake limetokea jana usiku.

Alisema ndege hiyo ilikuwa njia moja kuelekea Dar es salaam, kubainisha kuwa mtu huyo ndiye aliyeigonga ndege hiyo.

"Ingawa ndege ndio ilimgonga mtu huyo ambaye jina lake hatulifahamu, kisheria mtu au kitu chochote kinachokuwa kwenye njia ya kurukia na kutua ndege ndiyo kinahesabiwa kuigonga ndege. Ni kama ilivyo treni", amesema Mayongela.

Amesema kabla ya ndege hiyo kuruka, taratibu zote za kiusalama zilifuatwa ikiwemo kukagua njia kujiridhisha hakuna chochote.

"Haijulikani mtu huyo alitokea wapi, vyombo vya ulinzi na usalama vipo eneo la tukio kuchunguza tukio hilo kwa kina na tutatoa taarifa kamili uchunguzi utakapokamilika", amesema Kaimu Mkurugenzi huyo.

Amesema kitendo cha mtu huyo kuwepo katika njia ya kurukia ndege licha ya ukaguzi kufanyika kinawaumiza vichwa viongozi na wataalamu wa usalama uwanjani hapo.

"Pengine tatizo la muda mrefu la kukosa uzio tunaloanza kukubaliana nalo kwa ujenzi na upanuzi wa uwanja linaweza kuwa chanzo cha mtu huyo kuingia njia ya kurukia ndege", amesema.

Ili kukabiliana na matukio ya aina hiyo, amesema wataimarisha mifumo ya usalama kwenye viwanja vya ndege nchini.

No comments:

Post a Comment

Popular