Kampuni yauza shamba lake ili kuinusulu benki yake isifungwe na BOT. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 17 January 2018

Kampuni yauza shamba lake ili kuinusulu benki yake isifungwe na BOT.

Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU) kimetangaza kuuza shamba lake ili kuinusuru Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) baada ya Benki Kuu (BoT) kuitaka itimize sharti la kisheria la kuwa na mtaji cha Sh5 bilioni ndani ya miezi sita.

Wakati KNCU ikitangaza kupiga mnada mali hiyo, wateja wamepokea tangazo hilo la BoT kwa hisia tofauti, kutokana na baadhi kuanza kumimika kuchukua fedha zao wakihofia benki hiyo kufungwa.

Kwa wiki moja sasa, wateja wa KCBL wamekuwa wakimiminika kuchukua fedha zao, hali iliyosababisha uongozi kuweka kiwango cha ukomo cha Sh2 milioni kwa mteja mwenye zaidi ya Sh50 milioni.

KCBL ina wana hisa 245 ambao ni pamoja na vyama vya ushirika vya mazao (Amcos) na vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (Saccos) pamoja na watu binafsi 307 na inatoa huduma katika wilaya sita.

KCBL ni miongoni mwa benki tatu ambazo zilitangazwa na BoT Januari 4 kuwa zimepewa miezi sita kukidhi matakwa ya kisheria ya kuongeza mtaji hadi kufikia Sh5 bilioni.

KNCU inamiliki asilimia 69 ya hisa za benki hiyo na mwenyekiti wa chama hicho, Aloyce Kitau alisema jana kuwa wamelazimika kuuza shamba lao lenye ukubwa wa hekari 581 ili kuongeza hisa.

Kitau alisema mauzo ya shamba hilo la Lerongo lililopo wilayani Siha, yanatazamiwa kuingiza mapato ya Sh5 bilioni zitakazoingizwa KCBL.

Alisema mchakato wa uuzaji wa shamba hilo unaendelea na wana uhakika hadi kufikia Juni, ambao ni muda wa mwisho wa agizo hilo la BoT, watakuwa wameliuza.

“Tulipokea taarifa kuhusu upungufu wa mtaji na kwa kutambua umuhimu wa benki hii, wanachama wetu waliridhia kuuza hili shamba ili kuongeza mtaji wa benki,” alisema Kitau.

Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KCBL, Tumaini Yarumba aliwaomba radhi wateja ambao walipata taharuki na kushindwa kupata huduma za kifedha kwa wakati.

Alisema wamepewa muda hadi kufikia Juni wawe wamefikia mtaji unaohitajika na BoT na kwamba kwa sasa wanaendelea na juhudi za kukidhi vigezo.

“Tunaomba muendelee kuwa na imani na uvumilivu wakati benki inapowahudumia kwa nyakati tofauti, hasa ikizingatiwa muda tuliopewa na Serikali ni mrefu kwa benki hii kujiimarisha,” alisema

Meneja mkuu wa KCBL, Joseph Kingazi alisema tangu BoT ilipotoa tangazo hilo, wateja wao walikumbwa na taharuki na baadhi kukimbilia kutoa fedha zao kwa hofu kuwa inaweza kufungwa.

“BoT ilipotoa tangazo, wateja wengi walikuja tulianza kuwahudumia waliotangulia, lakini kuna ambao walionekana kukosa uvumilivu walipokosa fedha kwa wakati,” alisema.

Alisema jitihada za kuongeza mtaji zinaendelea na kusisitiza kuwa benki hiyo haitakufa.

No comments:

Post a Comment

Popular