Chadema njia panda uchaguzi wa Kinondoni. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 17 January 2018

Chadema njia panda uchaguzi wa Kinondoni.

 
Chadema, ambayo pamoja na vyama vingine vitano vilisusia uchaguzi mdogo katika majimbo matatu, sasa ipo njiapanda kusimamisha wagombea katika majimbo ya Kinondoni na Siha.

Wakati bado hakijatangaza kubadili msimamo huo, uongozi wa ngazi ya Wilaya ya Kinondoni umeanza kutoa fomu kwa ajili ya mchakato wa kupata mgombea kwa maelezo kuwa umeruhusiwa na uongozi wa juu wa chama hicho kikuu cha upinzani.

Lakini uongozi huo wa juu umesema bado haujafanya uamuzi kuhusu kushiriki uchaguzi katika majimbo hayo uliopangwa kufanyika Februari 17 na msimamo huo unaweza kutolewa wakati wowote. 

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Itifaki wa Chadema, John Mrema alisema jana kuwa wameunda kamati ndogo inayofanya utafiti kuhusu mchakato huo na kwamba uchukuaji fomu huo bado haujapewa baraka za ngazi za juu.

“Hatuna uamuzi wowote hadi sasa, ingawa ule wa awali wa kutoshiriki bado upo,” alisema Mrema.

“Lakini leo uamuzi utatoka. Bado tupo katika mjadala.”

Majimbo hayo mawili yanarudia uchaguzi baada ya waliokuwa wanayashikilia Maulid Mtulia (CUF, Kinondoni) na Dk Godwin Mollel (Chadema, Siha), kujiuzulu nafasi zao kwa nyakati tofauti na kuhamia CCM mwezi uliopita.

Mtulia alitangaza kujiuzulu ubunge Desemba 2 mwaka jana akisema hakushawishiwa na mtu yeyote, bali amebaini kuwa Serikali ya CCM inafanya kazi kubwa ya kutekeleza ilani yake na inafanya vizuri katika mambo mengi ambayo upinzani uliahidi kuyatekeleza.

Wakati Mrema akisema bado wanajadili ushiriki wa Chadema, uongozi wa Wilaya ya Kinondoni umeshaanza mchakato wa kupata mgombea wa kumrithi Mtulia ambaye mwaka 2015 alisimamishwa na vyama vinne vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutokana na makubaliano maalumu.

Uongozi huo umesema utasimamisha mgombea atakayepambana na Mtulia aliyepitishwa na CCM kuwania tena kiti hicho.

Mwenyekiti wa Chadema wa Kinondoni, Waziri Muhunzi aliongea na chombo kimoja cha habari nchini Jana kuwa baada ya kutafakari kwa kina na kuona mwenendo katika uchaguzi uliopita wa marudio katika majimbo matatu, wameamua kuanza mchakato wa kumsimamisha mgombea.

“Chadema wilayani Kinondoni, ndio tulioamua kuuomba uongozi wa juu kusimamisha mgombea wa jimbo hili na tuna imani litarudi mikononi mwa Ukawa,” alisema.

“Ingawa jambo hili halikuwa rahisi, nawashukuru viongozi wa juu kwa kutuelewa na kuturuhusu.

“Ugumu ulikuwapo kutokana na msimamo wa viongozi wa juu kuhusu malalamiko yao waliyoyatoa huko nyuma kuhusu uchaguzi wa kata 43. Hata hivyo, uchaguzi wa majimbo matatu tumeona baadhi ya mambo yameanza kufanyiwa kazi ikiwamo polisi kutoingilia.”

No comments:

Post a Comment

Popular