Utata waibuka baada ya serikali kukabidhi milioni 2 badala ya milioni 6 za msaada wa majeruhi 43 wa Bomu Kagera. - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 12 December 2017

Utata waibuka baada ya serikali kukabidhi milioni 2 badala ya milioni 6 za msaada wa majeruhi 43 wa Bomu Kagera.

Umeibuka mvutano mkubwa wa kugombea fedha za matibabu ya majeruhi 43 wa bomu la kurushwa kwa mikono lililosababisha vifo vya wanafunzi watano katika shule ya msingi Kihinda baada ya uongozi wa serikali ya wilaya ya Ngara mkoa wa kagera kukabidhi kiasi cha shilingi milioni mbili Badala ya shilingi milioni Sita zilizotolewa msaada kulipa deni katika hospitali ya misheni Rulenge Ngara.

Fedha hizo zimezua utata mkubwa baada ya katibu wa afya katika hospitali ya Rulenge Bi.Cartas Barnabas kupokea kiasi cha shilingi Milioni mbili badala ya shilingi milioni sita iliyotolewa msaada na kanisa la Anglikan Tanzania Dayosisi ya Kagera kupitia kitengo chake cha kuhudumia jamii Tumain Fund kwa lengo la kusaidia serikali kulipa deni la matibabu kwa majeruhi walionusurika katika ajali ya bomu la kurushwa kwa mikono hivi karibuni.

Awali akikabidhi msaada wa fedha kiasi cha shilingi Milioni sita na vifaa vya shule kwa majeruhi 43 wa shule ya msingi kihinda mratibu wa shirika la kuhudumia jamii Tumaini Fund wilayani Ngara Bw.Samoya Nyamkara amesema kuwa shirika la Tumain Fund limeishatoa misaada ya shilingi milioni 13,700,000 kwa majeruhi hao.

Akitoa ufafanuzi wa fedha hizo katibu tawala wilaya ya Ngara Bw.Vedastus Tibaijuka amesema kuwa kati ya fedha zilizotolewa msaada kulipa deni la hospitali ya Rulenge pia zitatumika kuhudumia majeruhi watatu waliohamishiwa hospitali ya Kagondo wilayani Muleba kwa lengo la kuwekewa macho bandia na wengine kuwekewa mboni ya jicho.

No comments:

Post a Comment

Popular