Watu wanaoishi jirani na makaburi wanaona mambo mengi - KULUNZI FIKRA

Sunday 5 November 2017

Watu wanaoishi jirani na makaburi wanaona mambo mengi

 Maeneo ya makaburi yanatisha, hasa nyakati za usiku na kuibua imani kuwa huenda mizuka huibuka usiku na kufanya mambo yao.
Hali hiyo ya utulivu na kutokuwa na harakati nyakati hizo, inatumiwa kama fursa na watu wengine; waganga, watambikaji na wengine watafuta bahati-bila kusahau wahalifu.

Wakazi wanaoishi pembeni mwa maeneo hayo ya kuzikia wafu wanaona mengi, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika maeneo mbalimbali.
Lakini ukosefu wa maeneo ya makaburi pia unasababisha adha kwa majirani wa maeneo hayo kwa kuwa nyumba hizo za wafu ‘zinawafuata’ wasipokuwa makini na wachimbaji.

Katika makaburi ya Mbuyuni, Tandika wilayani Temeke, ambako mwandishi alikuta familia ikilinda eneo lao lisigeuzwe kaburi.
“Tunakaa hapa kuwadhibiti hawa wachimba makaburi, bila hivyo unakuta kaburi jipya limechimbwa nje ya nyumba,” anasema Zuhura Hussein ambaye ni mama wa makamu.

Lakini, Hussein, ambaye ameishi eneo hilo tangu mwaka 1985, ameona mengi zaidi ya hayo ya wachimbaji kuvamia maeneo.
“Watu huwa wanakuja wakati mwingine mchana. Wanaoga na wanaacha hapohapo nguo walizoogea, wakati mwingine kaniki, shuka nyekundu na nyeupe,” anasema.

Anasema awali walitishika, lakini sasa wamezoea kwa sababu hilo eneo limekuwa njia na watu wengi wanapita. Pia, anasema wapo wanaokwenda na vichwa vya mbuzi na kondoo na kuvifukia makaburini.

Zuhura anasema wiki iliyopita alikwenda mtu aliyelowa damu akiwa na kichwa cha kondoo mkononi na kila anapokanyaga aliacha matone ya damu na kukifukia makaburini.

“Alivyomaliza kukifukia akaja kuomba maji ya kunawa,” anasema na kwamba walipoumuuliza sababu za kufanya hayo, alisema wanajaribu kuua kesi iliyopo mahakamani.

Zuhura haamini kama wanafanikiwa, lakini anasema “kila mmoja na imani yake. Kwa jinsi watu wanavyomiminika inawezekana wanapata matokeo halisi.”

Mkazi mwingine anayeishi jirani na makaburi ya watoto Temeke, Mohammed Hassan anasema kukithiri kwa vitendo vya ushirikina katika eneo hilo kulisababisha wananchi kukata mti uliokuwepo eneo hilo.

Anasema kulikuwa kukining’inizwa matambara ya rangi nyeupe, nyeusi na nyekundu na kukiwa na karatasi vyeupe zenye maandishi.
“Siogopi labda usiku mara mojamoja kwa sababu nimezaliwa hapa na makaburi nimeyakuta,” anasema.

Hussein anasema mara nyingi usiku wa manane huwa wanahisi mtu akitembea nyuma ya nyumba yao kuelekea makaburini.
Naye Mariamu Ulugulu anayeishi jirani na Zuhura, anasema wamekuwa wakivuta harufu ya ubani na udi uliochomwa.

Naye amekumbana na tishio la eneo lao kuchimbwa kwa ajili ya kuzikia.
“Unaona kaburi hili (anaonyesha kaburi lililopo karibu na nyumba yao). Lilichimbwa tulivyokwenda kumzika baba,” anasema.

“Haya mengi yaliyo jirani yote yalichimbwa tulipoondoka kidogo, hivyo tunalazimika kila tukitoka nyumbani abaki mtu kwa sababu wanaweza kuchimba hata hapa uani.”

Mkazi mwingine, Rapahel Mkotya anayeishi jirani na makaburi ya Mbagala Misheni anasema licha ya uangalizi ulipo bado kuna watu huenda kufanya kafara.

“Utaona wanaoga hapa, wanalala juu ya kaburi wengine wanaelekezwa walale chali, wengine kifudifudi wake kwa waume, ilimradi kila mmoja na lake,” anasema Mkotya.

Utapeli wa kiganga
Lakini pia maeneo ya makaburini hutumiwa kwa utapeli, kwa mujibu wa Mariamu Ulugulu, ambaye anasema wajanja hao hujidai waganga wa dawa za asili.

Huku akicheka anasema: “Mara kadhaa anapita kijana au mtu mzima anakwenda nyuma ya mbuyu, anajivisha nguo nyingi na anavaa kofia kubwa.

“Baada ya muda anapita mtu, mara nyingi ni wanawake. Akikaribia mwanzo wa makaburi eneo hili tulilokaa, anaambiwa kwa sauti ya kukwaruza na kutisha, ‘njoo kinyume nyume. Ndiyo tumesikia shida zako, weka hela hapo chini usigeuke kutazama mizimu. Tutakusaidia, una mitihani mingi umeibeba. Ondoka kwa usawa ulioelekea.”

Mariamu anasema baada ya mteja kuondoka anayesadikiwa kuwa mganga huvaa nguo za kawaida na kuondoka na anapopita nyumbani kwao huwaaga.

Anasema wapo ambao hufika maeneo hayo wakiwa na matenga yenye kuku na huzungumza lugha ambazo anasema hawazielewi na baadaye huyaacha makaburini.
Mariamu anasema wanapoamka asubuhi hukuta matenga matupu na kuku wakiwa wameshachukuliwa.

“Wakati mwingine wanafunga kuku kwenye miti hapa makaburini na baadaye kuku hukata kamba na kukimbilia mtaani,” anasema.
Anasema baadhi ya wanaochimba makaburi huokota kaniki na mashuka mekundu yanayoachwa makaburini, pia wapo ambao huchukua kuku wanaowakuta maeneo hayo.

Makaburi kujaa

Wakazi hao pia wamesema wamekuwa wakishuhudia wachimba makaburi wakivunja mabaki ya miili na kuhamisha ili kuwezesha kuzika maiti nyingine.
“Mara nyingi wanapochimba kaburi hupasua lile la awali, hivyo kwa bahati mbaya siku nyingine wanakuta nywele na mifupa, au wakati mwingine miili inatoa harufu,” anasema Mariamu.

“Hutuonyesha nywele, au huambiana wenyewe kwa wenyewe duh... nywele zinachelewa kuoza na wakati mwingine hutoa mifupa na kuiweka pembeni. Wakimaliza kuchimba kaburi jipya, huichimbia pembeni na kuifukia upya.

“Kuna kijana alikuwa anapita njia aliwahi kuokota mfupa wa mguu kuanzia gotini hadi kwenye nyayo na kusema anakwenda kuupamba ndani kwake kama fenicha.”

Makaburi kugezwa dampo

Jirani mwingine wa maeneo ya makaburi ya Kwa Kindale, Mtoni Mtongani anayeitwa Monica Lazaro anasema makaburi hayo yanawapa tabu ya kuzoa taka kila siku kutokana na kugeuzwa jalala.

Anasema wauza samaki na mizoga ya aina mbalimbali huitupa eneo hilo, hivyo kuwalazimu kuifukia ili kuepuka harufu.
Monica anasema pia wanaotumia dawa za kulevya hutumia makaburi hayo kujificha.

“Mara nyingi wanakuwa kule mwisho wa makaburi wakijichoma sindano na kusinzia kutwa nzima,” anasema Monica.

Anasema kulikuwa na mchimba kaburi aliyeitwa Kimwaki ambaye kila alipochimba na kukuta mifupa ya binadamu alituita kutuonyesha.
“Tulikuwa tunamkimbia. Mnaweza kwenda hadi mtaa wa pili kukaa kwa woga,” alisema.
“Akishatutisha ndiyo anaitenganisha na kuiweka pembeni kabla ya kuchimba shimo dogo pembeni ya hilo kaburi la awali na kuizika. Tulikuwa tunaogopa hadi tukazoea. Akianza kuchimba kaburi juu ya la zamani kila mtu anaingia ndani.”

Makaburi kuwa gesti

Mkazi aliyejitambulisha kwa jina la Nasra, ambaye madirisha ya nyumba yake yanapakana na makaburi ya Kinondoni, anasema eneo hilo limegeuzwa kuwa nyumba ya wageni, maarufu kama Guest Bubu.

“Huwa natamani nimwage upupu eneo lote hilo kwa sababu imekuwa kero. Watu hufika hapo jioni hadi asubuhi,” alisema.
Anasema angekuwa amepanga angehama kutokana na yanayoendelea eneo hilo.

“Unaona dirisha la chumbani nililiziba na nikatoboa huku mbele. Napata joto kwa sababu huku kumezibwa, lakini afadhali natulia kidogo,” alisema.

Sultani Athumani, mmoja wa vijana wanaolima mboga katika eneo la makaburi ya Chang’ombe ameshuhudia wengi wakifika eneo hilo kufanya kafara.

Anasema kwa hali ilivyo sasa katika makaburi hayo, kuna siku mafuvu yataelea na hasa kipindi cha mvua kwa sababu makaburi hufukuliwa, kuchimbwa na mabaki kuzikwa upya. “Wanafukua makaburi ili wachimbe mengine, kuna siku waliisahau mifupa bila kuifukia ikiwa na sanda yake tukaifukia,” anasema.

No comments:

Post a Comment

Popular