Shaka: Rais Magufuli hajawahi kutamka mahali popote kama serikali ni ya kwake. - KULUNZI FIKRA

Friday, 17 November 2017

Shaka: Rais Magufuli hajawahi kutamka mahali popote kama serikali ni ya kwake.

 
“Rais Dk John Pombe Magufuli hajawahi kutamka mahali popote kama Serikali ni ya kwake na si ya CCM kama ilivyodaiwa na kiongozi wa upinzani Bungeni Freeman Aikael Mbowe”, alisema Shaka.

“Pamoja na Serikali kuongozwa na Rais Magufuli bado iko chini ya Chama Cha Mapinduzi na kumtaka Mbowe kuacha maneno ya upotoshaji na uchochezi wa kitoto” - Shaka

“Rais Dk Magufuli tokea alipoingia madarakani miaka miwili iliopita amekuwa akihimiza shime ya kukuza fikra mpya na kudumisha uzalendo ulioporomoka na kuzaa kundi la mafisadi, wezi wa mali za umma bila kujali itikadi za kisiasa kwasababu uzalendo hauna alama ya siasa au chama”, alisema Shaka.

“Matamshi ya Mbowe hayana msingi wala mantiki yoyote bali anaonekana kama mtu anayeweweseka usingizini baadaa ya kuona utendaji wa Serikali ya CCM kwa miaka miwili ukiendeshwa kwa uwajibikaji, ufanisi, umakini na kuweka pembeni mitazamo hafifu ya kisiasa huku ikijali zaidi nchi na utaifa”, alisema Shaka.

"Mbowe ni mwanasiasa mnafiki na profesa wa kuzua. Amesahau alipowakusanya wananchi pale Mwembeyanga Temeke na kutaja orodha ya viongozi wa Serikali aliodai ni mafisadi likiwemo jina la Edward Lowassa aliyehamia Chadema na kuteuliwa kuwa mgombea urais", alisema Shaka.

“Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 /2020 ni miliki ya ya CCM na Rais Dk Magufuli hana ilani binafsi ya uchaguzi hivyo Mbowe aache kumlisha maneno Rais kwa kusaka kwake umaarufu dhaifu wa kisiasa", alisema Shaka.

"Mbowe aache kufuatilia mambo ya CCM kwasabahu hayatamsaidia yeye au chama chake. Hana sifa ya kuwa kiongozi mkweli mbele ya Watanzania kwa sababu ni wakala wa mafisadi na chama chake kimekuwa maficho ya viongozi wasiotamanika katika jamii", alisema Shaka.

“Serikali ya awamu ya tano haijawahi kukataa kupokea ushauri au maoni ndiyo maana Rais Dkt Magufuli amekubali hata kupokea ilani ya uchaguzi ya ACT Wazalendo na madai ya kuteua viongozi kwa mtazamo wa udini, ukabila au ukanda huo ni upuuzi usiohitaji kusikilizwa", alisema Shaka.

“CCM itaendelea kuamini na kufuata itikadi ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kama ilivyoanishwa kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani ujamaa si utitiri wa vibanda vya nyasi na kadhia ya umasikini bali ni imani na utekelezaji", alisema Shaka.

“Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kwa umakini na uangalifu mpya ili kukwepa yaliotokea nyuma yasijirudie tena na kukuta faida au tija ya rasilimali za Taifa zikiwanufaisha Mabepari na Mafisadi", alisema Shaka.

“Ninachokiamini kwa mujibu wa ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, Serikali haijaibeza sekta binafsi, kupuuzia uwekezaji na wawekezaji au kutofungua milango ya ushirika wa maendeleo bali kinachowatatiza baadhi ya Mafisadi na Wanasiasa uchwara ni kuzibwa kwa mirija na mianya ya wizi wao", alisema Shaka.

"Kiongozi yeyote anayekuwa wa kwanza kuumwa au kuthubutu kuutaja udini na ukabila hadharani huyo ndiye mkabila na mdini halisi. Hatuwezi kuteua viongozi kwa kutazama idadi ya makabila, dini au ukanda kwasababu Serikali si kilenge cha mizimu na matambiko", alisema Shaka.

“Nasikitishwa na matamshi ya Mbowe kudai hali ya uchumi ni mbaya wakati takwimu za uchumi katika taasisi za kitaifa na kimataifa zikiutaja uchumi wa Tanzania kukua kwa kasi", alisema Shaka.

"Huwezi kuwahimiza waumini wa Kikristo au Waislam kufanya ibada ikiwa hakuna Misikiti au Makanisa. Tunajenga viwanda, tutazalisha ili kupata masoko ya ndani na nje kutokana na ubora wa bidhaa. Hata Wachina, Waingereza na Wamarekani hatukukubaliana kama tutanunua bidhaa zao", alisema Shaka.

“Rais Magufuli na Seikali inayoongozwa na CCM itaendelea na mikakati yake katika dhamira ya kujenga uchumi imara wa viwanda kuelekea uchumi wa kati, kuziba mifereji ya wizi na ufisadi bila kuyumbiswa na mayowe ya wapinzani", alisema  Shaka.

Shaka Hamdu Shaka ni Kaimu Katibu Mkuu UVCCM ameyasema hayo alipozumgumza na waandishi wa habari ofisini kwake huko Upanga jijini Dar es Salaam kufuatia madai ya Mbowe dhidi ya Rais na utawala wake.

No comments:

Post a Comment

Popular