Mtatiro: Rais Magufuli hatakiwi kutamka hadharani kuwa haki za binadamu sio kipaumbele chake. - KULUNZI FIKRA

Saturday, 11 November 2017

Mtatiro: Rais Magufuli hatakiwi kutamka hadharani kuwa haki za binadamu sio kipaumbele chake.

Rais wa nchi anaposimama hadharani na kutamka kuwa kuwa yuko tayari kudharau kabisa HAKI ZA BINADAMU ili apambane na rushwa, inaonesha ni jinsi gani mtu huyu hajui anachosema na kwa hiyo anachofanya hakijui kabisa.

Kupambana na rushwa ni kuvipa vyombo na taasisi za kupambana na rushwa uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa nguvu kubwa na kila mwananchi avisaidie.
Kupambana na rushwa siyo Kuua uhuru wa kutoa maoni nchini mwako, kupambana na rushwa siyo kuliweka bunge mfukoni, kufungia magazeti yanayokuelezeni ukweli siyo kupambana na rushwa.

Kupambana na rushwa siyo kudharau amri za mahakama na kubomoa nyumba za wananchi huku mahakama imezuia. Kupambana na rushwa siyo kuzuia shughuli za kisiasa za vyama vyote huku wewe kila siku uko barabarani unafanya mikutano na wananchi kila unavyotaka.

Unapotamka hadharani kuwa HAKI ZA BINADAMU siyo kipaumbele chako inaonesha ni jinsi gani nchi yako inavyougua. It means hujali chochote kuhusu haki za msingi za raia wako, hujali chochote kuhusu raia wanaopotezwa kwa kutekwa (na vyombo vya dola vikituhumiwa kuhusika), hujali kuhusu wanasiasa wanaopigwa risasi ati kwa sababu wanatoa mawazo tofauti na fikra zako na kwa kweli una-PROVE kuwa HULINDI na KUHESHIMU katiba ambayo uliapa kuilinda na kuitetea.

Kwa kweli, iko siku utatutamkia kuwa wewe ni RAIS WA MILELE na kukuamini ni sawa na kuchota maji mtoni ili kuijaza bahari. Kauli hizi za Rais wetu John Pombe Magufuli juu ya Rushwa VS Haki za Binadamu, imenifanya niugue zaidi, kuwa Tanzania inarudishwa miaka 50 nyuma kama alivyowahi kutamka Jenerali Ulimwengu.

Lakini kama Taifa, sisi ndiyo Tanzania, Tanzania haitakuwa mtu, itakuwa watu, na watu ni sisi na tutaipigania Tanzania yetu dhidi ya mtu yeyote anayetaka Tanzania iendeshwe kwa mujibu wa akili na mawazo yake na utashi wake, na siyo katiba na sheria zetu.

No comments:

Post a Comment

Popular