Mke wa Tundu Lissu atoa ya moyoni kuhusu waliofanya shambulio. - KULUNZI FIKRA

Monday, 20 November 2017

Mke wa Tundu Lissu atoa ya moyoni kuhusu waliofanya shambulio.

Mke wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema angependa kuwajua watu waliomshambulia mumewe, aliyewaamuru wafanye shambulio hilo na sababu za kufanya uovu huo.

Mke huyo ambaye pia ni wakili, Alicia Magabe anasema kuwafahamu watu hao ni muhimu kwa kuwa familia haijui kwa sasa watu hao wanatafakari na kupanga kitu gani baada ya jaribio la kwanza la kumuua kushindikana.

Lissu, mmoja wa wanasiasa wasio na hofu kusema lolote wanaloliamini, alishambuliwa na watu wasiojulikana Septemba 7 akiwa ndani ya gari lililokuwa limewasili kwenye makazi yake Area D mjini Dodoma akitokea bungeni.

Tangu wakati huo, wakili huyo wa kujitegemea na mwanasheria mkuu wa Chadema, amelazwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na hadi sasa Jeshi la Polisi halijaeleza kama limeshapata fununu ya waliohusika zaidi ya kujibu kuwa linaendelea na upelelezi kila waandishi wanapotaka kujua maendeleo ya suala hilo.

Na sasa mke huyo wa Lissu na ambaye pia ni wakili, Alicia Magabe anataka kuwajua waliomfyatulia mumewe zaidi ya risasi 30, aliyewatuma na sababu za kuwatuma.

Magabe pia anasema familia yake kwa sasa ipo shakani kwa kuwa hajui hao waliofanya shambulio hilo ambalo linaonekana la kukusudia kumuua, wanatafakari nini na kupanga nini.

Akizungumza na Mwananchi katika Hospitali ya Nairobi, Wakili Magabe alisema Lissu ametumia sehemu kubwa ya ujana wake kupigania masilahi na haki za Watanzania, hivyo angependa kuona haki inatendeka.

“Binafsi nimewasamehe kwa kitu walichokifanya, lakini hiyo haina maana kwamba nisingependa kuona haki inatendeka,” alisema wakili huyo.

“Sitaki kuwe na mkanganyiko baina ya kusamehe na hali ya kutamani kuona haki inatendeka.”

Alisema tukio hilo limemfanya aanze kuamini kuwa kuna watu walitaka kumuua Lissu, lakini hawajafanikiwa na anaamini watu hao wapo, hivyo anahofia usalama wa familia yake.

“Mpaka sasa sijasikia kama kuna uchunguzi wowote umefanyika na sijawahi kusikia watu wamekamatwa,” alisema Wakili Magabe.

“Hivyo nawaza kuwa hayupo salama na mimi kama mke wake sijisikii kama niko salama sana. Nawaza hawa watu watakuwa wanatafakari au wanapanga nini. Hiyo ndiyo hali niliyonayo kwa sasa. Sijui hao watu wako wapi.”

Hata hivyo, Wakili Magabe alisema Lissu yuko imara na shambulio hilo halijamrudisha nyuma katika harakati zake za kupigania haki na za kisiasa.

Alisema hilo alilionyesha mara tu alipopata fahamu.

“I have survived to tell a tale, I have lived to tell a tale (nimeepuka kifo ili nieleze jambo) ndivyo alivyosema baada ya kuzinduka,” alisema Wakili Magabe.

Alisema baada ya fahamu kumrejea sawasawa amekuwa akizungumza maneno yanayoashiria kwamba ana ari zaidi.

“Spirit yake ipo very high (ari yake iko juu sana). Si mtu wa kusema kuwa baada ya tukio amekuwa mnyonge, mwoga au ujasiri wake umepungua,” alisema wakili huyo.

“Sijawahi kupata hata kauli yake moja inayoashiria kwamba sasa atarudi nyuma. Kama mke nataka mume wangu apone, tutoke hospitali turudi nyumbani. Lakini wanapokuja viongozi wenzake kutoka Tanzania; wastaafu na wa sasa na hata hapa Kenya, kauli zake zote zinaashiria amekua zaidi kisiasa.

“Anasema ‘kuna siku nitapona na nitaendelea na kazi zangu’ ili kuwatia moyo wanasiasa na wanaharakati.”

Kuhusu mumewe kuendelea na siasa baada ya kupona, Wakili Magabe alisema Lissu ndiye anaweza kulizungumzia suala hilo.

“Mimi nikiwa msaidizi wake wa kwanza, nitakuwa mtu wa mwisho kusema Lissu asifanye analotaka kwa kuwa hata akiyatamka hayatakuwa na nguvu mbele za Mungu,” alisema.

“Binafsi nasema alikuja duniani kwa makusudi. Mungu alimleta duniani kwa sababu na alijua hata kabla hajazaliwa maisha yake yatakuwaje na atafanya nini hapa duniani.

“Sidhani kama kuna binadamu anaweza kuzuia yale ambayo Mungu amepanga. Sitaki kusema kama ataendelea na siasa, hataendelea nazo, yupo kwa kusudi lake.”

Magabe alisema kuna watu wanapigwa risasi moja na wanafariki dunia, lakini Lissu alipigwa risasi 16 za moto ambazo zilipita kwenye mwili wake na anaendelea kuishi.

Alisema anafarijika kuona Lissu yu mzima kwa kutumia nguvu za watu wote ambao kwa namna moja au nyingine wanapenda aishi, akianzia na waliochanga fedha, waliomtolea damu, walioomba, waliomnyanyua, waliomtibu mara ya kwanza na wanaoendelea kumtibu.

“Hatujawahi kuwa peke yetu na nimegundua kumbe kupigwa risasi kwa Lissu ni tukio ambalo limewagusa Watanzania na mataifa mengi na wapo tayari kusaidia,” alisema mwanamke huyo.

“Hii ni kwa kuwa ametumia ujana wake kupigania masilahi na haki za Watanzania.”

No comments:

Post a Comment

Popular