Meya wa Iringa kwa tiketi ya Chadema afikishwa mahakamani kwa kutishia kuua kwa bastola. - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 28 November 2017

Meya wa Iringa kwa tiketi ya Chadema afikishwa mahakamani kwa kutishia kuua kwa bastola.

 
 Meya wa Manispaa ya Iringa (Chadema), Alex Kimbe amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa akikabiliwa na shtaka la kutishia kuua kwa bastola.

Kimbe anadaiwa kutenda kosa hilo Jumapili Novemba 26,2017 wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Kitwiru mjini Iringa.

Mwendesha mashtaka wa Polisi, Aristeck Mwinyekheri mbele ya Hakimu Mkazi, John Mpitanjia amedai leo Jumanne Novemba 28,2017 kuwa Kimbe alitishia kumuua katibu wa umoja wa vijana wa CCM (UVCCM), Iringa Mjini, Alfonce Muyinga kinyume cha sheria.

Kimbe amekana kutenda kosa hilo na ameachiwa kwa dhamana. Hakimu Mpitanjia ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 12,2017.

Wakati huohuo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imewasomea mashtaka matatu washtakiwa watano wanaodaiwa kujeruhi Novemba 19,2017 wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Kitwiru.

Washtakiwa hao katika kesi namba 190/2017 ni Martha Robert, Leonard Kulijira, Esau Bwire, Christopher Jevas na Samwel Nyanda.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Richard Kasele mwendesha mashitaka Chakila Felix amedai washitakiwa walijeruhi, kuteka na kufanya unyang’anyi kwa kutumia nguvu.

Washtakiwa wanadaiwa kumjeruhi Dick Frank na kumnyang’anya simu ya mkononi.
Kutokana na shtaka la unyang’anyi wa kutumia nguvu ambalo halina dhamana, washtakiwa wamepelekwa rumande na kesi itatajwa Desemba 12,2017.

No comments:

Post a Comment

Popular