Mbunge wa Mlimba chadema na wafuasi 41 wahamishiwa kituo kikuu cha polisi chini ya ulinzi mkali. - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 28 November 2017

Mbunge wa Mlimba chadema na wafuasi 41 wahamishiwa kituo kikuu cha polisi chini ya ulinzi mkali.

 
Mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga na wenzake 41 wamehamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro wakitokea wilayani Ulanga walikokuwa wakishikiliwa awali baada ya kukamatwa wilayani Malinyi.

Wakati wakifikishwa kituoni hapo Jana Jumanne Novemba 28,2017, ulinzi uliimarishwa, huku waandishi wa habari wakikatazwa kupiga picha.

Baadhi ya wanahabari walisukumwa ili kuondoka eneo hilo. Watuhumiwa hao wamefikishwa kituoni hapo saa 9:30 alasiri wakiwa kwenye magari matatu ya polisi.
Jumapili Novemba 26,2017 saa tano usiku watuhumiwa hao walikamatwa wakiwemo madiwani wawili wa Ifakara, wakituhumiwa kufanya fujo zilizohusisha uharibifu wa mali za umma.

Vurugu hizo zilitokea baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Sofi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei amesema hawezi kuzungumza lolote kuhusu watuhumiwa hao kwa kuwa bado wanawasubiri wengine kutoka wilayani Ulanga.

Katika taarifa ya awali, Kamanda Matei alisema watuhumiwa hao walichoma moto ofisi za taasisi za umma yakiwemo majengo ya shule ya msingi Sofi, ofisi ya mtendaji kata na nyumba ya walimu wa shule hiyo.

Kamanda Matei alisema pia wanaendelea kumtafuta mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali kutokana na tuhuma za kuhamasisha vurugu.

No comments:

Post a Comment

Popular