Lusinde amshambulia Lazaro Nyalandu kwa uamuzi wake. - KULUNZI FIKRA

Thursday 2 November 2017

Lusinde amshambulia Lazaro Nyalandu kwa uamuzi wake.

 Mbunge wa Mtera kupitia Chama cha Mapinduzi, Livingstone Lusinde Lusinde amesema kwamba aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu kuondoka kwenye chama chao hajaacha pengo kwani mwanasiasa huyo anafanya siasa zisizo na msisimko ingawa ana bahati.

Mbunge huyo amesema kwamba anamfahamu Nyalandu kama mwanasiasa 'Togwa' kwa sababu amekuwemo kwenye baraza la Mawaziri, Mjumbe Halmashauri kuu CCM taifa lakini tangu amemfahamu kuwa mjumbe wa NEC hajawahi kusimama kwenye kikao chochote cha NEC na kuuliza chochote ingawa ana bahati lakini siasa zake hazina msisimuko.

"Namfahamu Nyalandu kama mwanasiasa Togwa, mwanasiasa aliepoa na hana msisimko lakini mwenye bahati, ana bahati kwa sababu amekuwemo kwenye baraza la mawaziri, mjumbe halmashauri kuu CCM taifa lakini tangu nimfahamu kuwa mjumbe wa NEC hajawahi kusimama kwenye kikao chochote cha NEC. Kuondoka kwake hakujaacha pengo CCM bali ameacha fursa kwa mwanachama mwingine kupata nafasi" amesema Lusinde.

Aidha Lusinde amefafanua kwamba  katika hoja sita za Nyalandu zilizomsababisha yeye kuamua kuondoka CCM hoja yake kubwa ni kuwa serikali inakigandamiza chama na kushindwa kuisimamia serikali, kitu ambacho amesema kiongozi huyo alikuwa akiizungumzia  CCM ya mwaka 75 ambayo katibu kata ndie alikuwa mtendaji wa kata na DC kuwa katibu wa CCM wa wilaya hivyo hakuna kimbilio mfumo ambao katika CCM mpya haupo.

"CCM mpya haijengwi kwa mtindo wa kukandamiza bali inajengwa kwa kuondoa siasa za hovyo za majukwaani  na kupeleka siasa za kazi ambazo pengine Nyalandu hajazizoea, katika hoja zake sita hakuna hoja ambayo inagusa wapiga kura wake ilimsababishia yeye kuhama chama.."amesema  Lusinde.

Hata hivyo Lusinde amezikosoa sisasa za Upinzani na kusema kwamba ni siasa za unga wa ngano kwani walikuwa wanamshambulia Nyalandu kabla hajahama kama kiongozi dhaifu na dhalili asiefaa lakini akijiunga na CHADEMA zitasikika sifa nyingi akimwagiwa.

No comments:

Post a Comment

Popular