Lazaro Nyalandu: Kuhama CCM ni miongoni mwa mambo matatu muhimu niyoyafanya katika historia ya maisha yangu. - KULUNZI FIKRA

Thursday 2 November 2017

Lazaro Nyalandu: Kuhama CCM ni miongoni mwa mambo matatu muhimu niyoyafanya katika historia ya maisha yangu.

 
 Aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu amesema hatua yake ya kujitoa CCM, ni moja ya mambo matatu makubwa aliyofanya maishani hadi sasa.

Nyalandu (47) pia amejibu uvumi uliozagaa katika mitandao ya kijamii kuwa ameamua kujiondoa CCM kutokana na kuanza kuchunguzwa, akisema hajawahi kuhojiwa na kikao chochote cha chama hicho kuanzia ngazi ya wilaya.

Nyalandu, ambaye amewahi kuwa naibu waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara na baadaye Maliasili na Utalii kabla ya kuwa waziri kamili, alitangaza uamuzi huo Jumatatu akisema haridhishwi na mwenendo wa kisiasa nchini, ukiukwaji wa haki za binadamu, dhuluma na mihimili miwili ya nchi kushindwa kufanya kazi yake kwa uhuru.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu jana, Nyalandu alitaja uamuzi mwingine mkubwa kuwa ni kumfuata Yesu Kristo awe mwokozi wa maisha yake kama dini ya Kikristo inavyotaka. Napia kuamua nani atafaa kuwa mke wake.

Nyalandu ni muumini wa makanisa ya Kikristo ya uamsho na alikuwa mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Wanafunzi wa Kikristo (Ukwata). Nyalandu amemuoa mshindi wa taji la urembo la Miss Tanzania mwaka 2004, Faraja Kota.

Alisema kuhama CCM ni kitu kilichomchukua muda mrefu kutokana na yanayoendelea ndani ya chama hicho tawala.

“Nimeutafakari (uamuzi huu) kwa zaidi ya mwaka. Wapo watu wanasema eti nimehama kwa kukosa uwaziri, hii si kweli. Nimechukua uamuzi huu si kwa sababu ya Lazaro Nyalandu bali kwa kuangalia maslahi mapana ya umma wa Watanzania,” alisema Nyalandu.

Alisema ameona kuna mmomonyoko wa tunu zilizomfanya awe CCM , kama kutokuwa na uhuru wa mawazo kama ilivyokuwa awali.

“Ule uhuru wa mawazo uliokuwepo unamomonyoka, demokrasia ndani ya chama inamomonyoka. Niliona pia tulikuwa na ulazima kama Taifa kupata Katiba mpya. Ile Rasimu ya Warioba niliikubali sana, lakini mchakato ulivyoendeshwa na kile kilichopatikana sikukubaliana nacho,” alisema Nyalandu.

Alisema kutokana na hali hiyo aliona ajiondoe CCM na kuungana na upinzani ambao haukukubaliana na mchakato wa Katiba baada ya maoni ya Warioba kuwekwa kando.

Nyalandu alisema katika vipindi vinne vya ubunge wake, alifanya kazi vizuri na wabunge wenzake na baadhi ya wanaCCM, lakini kama chama aliona kinakosa mwelekeo.

“Chama ni kama mashua au boti iliyokosa mwelekeo ndani ya maji. Hakiendi mashariki, magharibi, kaskazini wala kusini. Na kwa kuwa CCM ndiyo inaongoza Serikali yetu, nikaona huko tuendako si sahihi. Nilipoona hivyo nikaamua nihamie upande wa pili,” alisema Nyalandu.

“Ninaona kuna haja ya kupata Katiba ili tuweze kuwa na mipaka ya mihimili ya nchi; Bunge, Serikali na Mahakama. Tunataka kuwa na siasa za wazi. Bunge liwe live (lirushwe moja kwa moja na vyombo vya habari) watu walione na sheria iongoze nchi.”

Pamoja na wanasiasa wa upinzani kukabiliana na misukosuko dhidi ya vyombo vya dola, Nyalandu haoni kama atapata tatizo hilo.

“Tanzania ina watu milioni 50 na wote hao si wabunge wa CCM. Ninatarajia, kama wengine wote, nitalindwa na mawazo yetu yatalindwa na kusikilizwa. Tunayo haki ya kutoumizwa kwa namna yoyote na usalama wetu kulindwa,” alisema Nyalandu.

Kuhusu kugombea tena ubunge katika uchaguzi mdogo uliosababishwa na kujivua uanachama, Nyalandu alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa kwa kuwa bado anasikilizia hatma ya uanachama alioomba Chadema.

Alisema ameomba kujiunga na Chadema na bado anasikilizia uamuzi rasmi wa chama hicho ambacho pia kina mamlaka ya kuteua mtu wa kukiwakilisha kwenye uchaguzi huo.

Kuhusu madai kuwa ameamua kutoka CCM baada ya kuhojiwa kwa tuhuma mbalimbali, Nyalandu alisema hilo si kweli na hajawawahi kuhojiwa na kamati yoyote ya maadili, kuanzia wilaya, mkoa hadi Taifa.

Alisema hata zile tuhuma ambazo pia zimeanza kuibuliwa mitandaoni dhidi yake, si za kweli bali zinalenga tu kumchafua.

Alisema anashangaa tuhuma hizo kuibuliwa zaidi ya miaka miwili tangu aachie uwaziri na kueleza ni jinsi gani hahusiki.

Kuhusu utoroshaji wa twiga kwenda nje ya nchi, Nyalandu alisema tukio hilo lilitokea kabla hajawa Waziri wa Maliasili na Utalii na kuwa katika kipindi chake hakuna kitalu chochote cha uwindaji kilichotolewa.

Alisema vitalu huwa vinatolewa kisheria na vina muda wake, hivyo alipoingia wizarani alikuta vimeshatolewa na mtangulizi wake, Ezekiel Maige na muda ulifika tena katika kipindi cha Profesa Jumanne Maghembe wakati yeye ameshamaliza kipindi chake.

Kuhusu kashfa ya Faru John iliyoundiwa kamati na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Nyalandu alisema hilo lilihusu Bodi ya Ngorongoro na uchunguzi ulifanyika na likaisha.

Nyalandu aliwataka wanaosambaza kashfa hizo waache kwa kuwa si za kweli.

Kuhusu kutoaga jimboni, Nyalandu alisema kabla ya kujiuzulu alizunguka vijijini kuzungumza na wananchi na kukagua miradi ya maendeleo aliyoianzisha, lakini akasema katika siasa lazima kuwe na fursa ya kushtukiza, hivyo asingeweza kutangaza uamuzi huo katika mkutano wa hadhara.

No comments:

Post a Comment

Popular