Kenya na Tanzania zimeshindwa kufikia makubaliano katika mazungumzao ya kidiplomasia. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 8 November 2017

Kenya na Tanzania zimeshindwa kufikia makubaliano katika mazungumzao ya kidiplomasia.

 
 Waziri wa mambo ya nje nchini Kenya Amina Mohamed ameilalamikia serikali ya Tanzania kufuatia hatua ya taifa hilo kuwapiga mnada zaidi ya ng'ombe 1,300 walioingia nchini humo kinyume na sheria.

Serikali ya Rais John Magufuli ilichukua hatua hiyo baada ya wafugaji kuingia nchini humo na mifugo wao wakitafuta lishe.

Hatua hiyo inajiri siku moja tu baada ya Rais Magufuli kusema kuwa taifa hilo sio shamba la mifugo wa taifa jirani.

Hatua ya kuwapiga mnada ng'ombe hao ilizua hisia kali miongoni mwa wafugaji wa Kenya baada ya wenzao waliokuwa na mifugo hao kukamatwa na kuzuiliwa kwa kuingia nchini humo kinyume na sheria.

Na kufuatia hatua hiyo waziri wa mambo ya nje nchini Kenya Amina Mohammed alidaiwa kuanzisha mazungumzo kati ya serikali hizi mbili kutatua mzozo huo, mazungumzo ambayo yalishindwa kufua dafu.

''Tulidhani kwamba mazungumzo ya kidiplomasia yangetatua mzozo huu, lakini tulishindwa kuafikia makubaliano. Ni wakati huo ambapo tuliamua kuzungumza na balozi wetu nchini humo kuwasilisha barua ya kupinga hatua ya kuwapiga mnada mifugo hao''.

''Historia ambayo tumekuwa nayo na Watanzania ni nzuri sana na kila kunapotokea tatizo tumekuwa tukitatua.Ni kwa sababu hiyo ambapo imekuwa hatua ya kushangaza miongoni mwa wafugaji wa Kenya'', waziri huyo alizungumza katika mkutano na vyombo vya habari.

Bi Mohamed amesema kuwa Kenya imekuwa ikiwavumilia wafugaji wa nchi jirani ambao wamekuwa wakivuka na kuingia katika eneo la Kajiado nchini Kenya kwa wingi.

''Barua yetu ya pingamizi ni kuonyesha wasiwasi wetu kuhusu kisa kilichotokea licha ya kuwepo katika mazungumzo, tunatumai tutasuluhisha tatizo hili'', alisema waziri Mohamed.

No comments:

Post a Comment

Popular