Katibu wa ACT-WAZALENDO mkoa wa Dodoma na Wanachama 800 wahamia CCM. - KULUNZI FIKRA

Saturday 4 November 2017

Katibu wa ACT-WAZALENDO mkoa wa Dodoma na Wanachama 800 wahamia CCM.

 
 CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)mkoa wa Dodoma kimezindua kampeni kwa kishindo kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Chipogoro huku kikiwataka wakazi wa kata hiyo kuendeleza heshima iliyopo ya Dodoma kuwa ngome ya CCM.
ac.jpg ac1.jpg
Katika uzinduzi huo kimepokea kadi za Chama Cha ACT Wazalendo mia nane ikiwemo kadi ya aliyekuwa katibu wa chama hicho mkoa wa Dodoma Weston Kaduma.

Akizindua kampeni hiyo mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma alhaj Adam Kimbisa amesema siku zote Dodoma ni ya CCM hivyo watumie uchaguzi huo kumpa rais nguvu kwa kumchagua Hosea Fweda na kutoiyumbisha CCM.

“Juzi kuna chama kilikuja kuzindua kampeni zake hapa,kuna vijana walienda,nawapongeza vijana wale kwa kwenda kuwapa kampani lakini nina uhakika ndani ya mioyo yao wanasema wataipigia kura CCM, maana ndugu zangu mgeni akija kwako ukimuacha peke yake hatojisikia vizuri,”amesema Kimbisa.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde aliwataka wakazi wa Chipogoro kuimarisha umoja wao,kuepuka vurugu,kushauriana,kubishana kwa hoja na kumchagua diwani anayetokana na CCM ambaye ni Hosea Fweda.

“Ndugu zanguni mchagueni Hosea atetee shida zenu,awasilishe shida zenu kwa tajiri,sasa ukimchagua Jafari anapeleka wapi shida zenu kwa Mbowe?Mbowe apelekewe ana serikali?lakini ukimchagua Hosea awe diwani wa Kata hii kwa tiketi ya CCM atapiga mpira utapokelewa na mbunge,mbunge nae atapiga shuti kali mpaka golini ambapo ni kwa rais,”alisema Lusinde.

Kwa upande wake mgombea Fweda amewaomba wananchi wamchague ili ashirikiane nao katika kuwaletea maendeleo na kuahidi kuwa diwani wa Chipogoro katika kuwatumikia.

“Nichagueni mimi najua changamoto zilizopo katika kata hii ikiwemo ukosefu wa umeme,kituo cha afya na kwamba kwa kutumia viongozi na serikali ya CCM changamoto hizo tutazitatua,”alisema Fweda.


Mkoa wa Dodoma unafanya uchaguzi mdogo wa marudio katika kata moja ambayo ni ya Chipogoro.
 

No comments:

Post a Comment

Popular