Wakili augua gafla kesi ya bilionea Msuya - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 31 October 2017

Wakili augua gafla kesi ya bilionea Msuya

 
 Baada ya wakili wa utetezi, John Lundu kuugua ghafla na kushindwa kuingia kortini kumfanyia mahojiano shahidi wa 11 wa upande wa Jamhuri.

Licha ya Lundu kuugua, pia mawakili wengine wawili - Majura Magafu na Hudson Ndusyepo - wanaowatetea washtakiwa saba katika shauri hilo nao hawakutokea mahakamani na hivyo Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo kuamua kuahirisha shauri hilo hadi leo.


Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi 22 Agosti 7, mwaka 2013, majira ya saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kando kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Sharif Athuman (31), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo, mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha na Shaibu Saidi, maarufu kama Mredii (38), mkazi wa Songambele, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.

Wengine ni Mussa Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu, Jalila Said (28), mkazi wa Babati na Sadiki Jabir a.k.a Msudani (32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, wilaya ya Hai.

Washitakiwa wengine ni Karim Kihundwa (33), mkazi wa Lawate, wilaya ya Siha na Alli Musa maarufu Majeshi, mkazi wa Babati, mkoani Manyara.

Akiahirisha shauri hilo, Jaji Maghimbi alisema: “Mahakama imekubaliana na hoja ya upande wa mashtaka walioomba kesi hii iahirishwe hadi kesho (leo) kutokana na wakili Lundu kuugua na kushindwa kuendelea kumhoji shahidi wa 11 wa upande wa mashtaka ambaye ni detective (mpelelezi), koplo Seleman (Mwaipopo) ambaye bado yuko chini ya kiapo.”

Maelezo yaliyoandikwa na shahidi huyo yaliibua kesi ndani ya kesi katikati ya wiki iliyopita, kwa kuwa ndiye ofisa upelelezi aliyekuwa akifuatilia nyendo za washtakiwa hao kupitia mitandao ya simu za mkononi, baada ya kutekelezwa kwa mauaji hayo hadi walipokamatwa.

Kutokana na mgongano huo wa kisheria uliojitokeza, upande wa mashtaka umeita mashahidi wawili kumaliza mvutano huo ambao ni koplo mpelelezi Jawadu Mhenga na koplo mpelelezi Mwaipopo.

Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo namba 12 ya mwaka 2014, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula aliieleza mahakama hiyo kuwa mtu wa mwisho aliyekuwa amebakia kufanya mahojiano na shahidi wa 11 ni wakili Lundu wa upande wa utetezi.

“Taarifa tulizopokea kutoka kwa wakili Emanuel Safari ni kwamba mwenzao John Lundu amepata dharura na ameshindwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi hii kutokana na ugonjwa," alisema Wakili wa Serikali Chavula na kueleza zaidi, "ameugua ghafla na hawezi kuwapo mahakamani leo (jana)".

"Kutokana na hali hiyo na kwa kuwa alipaswa kufanya yeye cross examination (mahojiano) tunaomba mahakama yako tuahirishe shauri hili hadi kesho.”

Jopo la mawakili wa utetezi katika kesi hiyo linaongozwa na Ndusyepo anayemtetea mshitakiwa wa kwanza, Magafu anayemtetea mshitakiwa wa pili na wa tano, Safari anayemtetea mshitakiwa wa tatu na Lundu anayemtetea mshitakiwa wanne, sita na saba.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo ambayo ni gumzo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, unaongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Chavula.

Hadi sasa jumla ya mashahidi 10 wa upande wa Jamhuri wameshatoa ushahidi wao mahakamani hapo ambao ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Hai (OC-CID), Joash Yohana na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai (DMO), Dk. Paul Chaote (39) .

Mwingine ni Khalid Sankamula (49) ambaye ni mganga wa kienyeji na mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Limbula, wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.

Mashahidi wengine waliopita ni Anase Khalid (37), mkulima na mkazi wa Kaliua na Tabora na Mbazi Steven (32), mkazi wa Arusha.

Wengine ni Ofisa Upelelezi, Kitengo cha Intelijensia ya Jinai mkoa wa Kilimanjaro, Herman Ngurukisi (40), Inspekta Samueli Maimu (45) ambaye alikuwa kiongozi wa timu ya ukaguzi ya Polisi (CRT) kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upepelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa mkoa wa Kilimanjaro na Ofisa Upelelezi, Sajenti Atway Omari ambaye alikuwa katika timu ya CRT.

Kesi hiyo itaendelea tena leo.

No comments:

Post a Comment

Popular