Serikali imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti la Tanzania Daima kwa kipindi cha siku tisini (90) ikiwa sawa na miezi mitatu kuanzia leo.
Kufungiwa huko kunakuja kufuatia gazeti hilo kuandika habari zilizothitishwa kuwa ni uwongo na kufanya upotoshaji uliodaiwa kuleta taharuki huku likikiuka kifungu cha Sheria 54(1) cha sheria ya Huduma za Habari Na.12,2016 baada ya kuandika taarifa iliyotoka kwenye toleo la 4706 la Oktoba 22,2017 kuwa: "Asilimia 67 ya WatanzaniaWanatumia ARVs". Na kisha kuomba radhi.
Mbali na upotoshaji huo kwa Umma, gazeti hilo limedaiwa kuonywa mara kwa mara na kuomba radhi lakini limekuwa likiendelea kutenda makosa hayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi tangu mwaka jana gazeti hilo limeshafanya makosa ya kunukuu vibaya na baadhi ya viongozi akiwemo, waziri wa viwanda na biashara na kushindwa kuthibitisha, mwanasheria mkuu wa Serikali, George Masaju ambapo mhariri alipoulizwa kuhusu nukuu hizo alikiri kutotamkwa na kiongozi huyo.
Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa, gazeti hilo limekuwa likiandika habari zenye vichwa vya habari zilizojaa, kejeli na dharau kwa serikali.
Serikali, kupitia waziri wa habari, imewaonya waandishi na wahariri wa habari kusimamia wajibu na kufuata misingi ya taaluma na sheria ya taaluma yao.
No comments:
Post a Comment