Mkuu wa wilaya ya Arumeru akiri kuwanunua madiwani wa chadema - KULUNZI FIKRA

Thursday, 26 October 2017

Mkuu wa wilaya ya Arumeru akiri kuwanunua madiwani wa chadema

 
 Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, amesema wana uwezo wa kuwanunua madiwani wote 20 wa CHADEMA ili Halmashauri hiyo iendeshwe na CCM, na kwamba Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, naye kama anataka aende atanunuliwa kwa hela nyingi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mnyeti kuzungumza tuhuma zilizotolewa na Nassari na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kuwa DC huyo amekuwa akinunua madiwani wa CHADEMA kwa Sh milioni mbili.

Jana akiwa katika Kata ya Sambasha iliyopo wilayani Arumeru, mara baada ya kumaliza kutatua mgogoro wa maji kati ya Kata hiyo na Shamba la Miti la Meru, Mnyeti alisema; "Acha nijibu kidogo maana kuna vyombo vya habari hapa, msije mkanukuu vibaya, moja ni hili la madiwani kununuliwa, walionunuliwa inasemekana wako sita, bado hawajatosha.

"Nahitaji kununua 20, ili wawe 26, uchaguzi turudie kata zote, kwahivyo na wale ambao wanataka kununuliwa nao tunawakaribisha, fedha tunazo.

"Na tuko tayari kuwanunua mwisho wa siku tunataka Halmashauri yote iwe ya CCM, CCM hoyee. 'Message sent', uongo kweli? Kwa hiyo kama ni kununua, wacha niondoe hii habari ya kelele ndogo ndogo za pembeni, wanaotaka kununuliwa karibuni.

"Na yeye Mbunge Nassari kama anataka kununuliwa naye tunamkaribisha, kwa kuwa ni mbunge, eneo lake ni kubwa zaidi, basi yeye tutamnunua kwa hela nyingi zaidi, kwa hiyo yeye kama yuko tayari basi aje tutamnunua kwa fedha nyingi zaidi. Sambasha hoyee".

No comments:

Post a Comment

Popular