Jeshi la polisi linawashikilia askari wawili wa FFU kwa tuhuma za kupiga wananchi ukonga - KULUNZI FIKRA

Thursday, 26 October 2017

Jeshi la polisi linawashikilia askari wawili wa FFU kwa tuhuma za kupiga wananchi ukonga

 
Wakati Jeshi la Polisi likiwashikilia askari wawili wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwa tuhuma za kuwapiga wananchi wa eneo la Ukonga, tayari watu zaidi ya 40 wameitikia wito wa kuwataka waorodheshe majina yao ofisi ya ofisa mtendaji wa Kata ya Ukonga kutambuliwa kuwa walipigwa katika vurugu hizo.

Wito huo ulitolewa na mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema aliyeenda eneo hilo juzi asubuhi kuzungumza na wananchi waliofunga barabara na kuandamana kupinga uovu huo wa askari.

Wananchi hao wanadai kuwa askari wa kikosi hicho kutoka kambi iliyopo Mombasa, wamekuwa wakiwapiga na kuwapora mali kuanzia Ijumaa hadi juzi baada ya askari mwenzao, Charles Yanga kukutwa ameuawa nje ya kambi.

Akizungumza na gazeti hili jana, ofisa mtendaji wa Kata ya Ukonga, Eligius Mlokozi alisema hali ni shwari kwa sasa na tayari wananchi wamejitokeza kujiorodhesha.

“Mpaka asubuhi hii ya leo (jana saa 5:00), tumepokea watu 29 ambao wamedai kuibiwa na kuharibiwa mali zao na watu 11 ambao wamedai wamejeruhiwa. Na bado tunaendelea kukusanya majina mengine,” alisema.

Alisema tangu Mjema alipotoa agizo, ofisi yake haijapokea taarifa yoyote inayoashiria kuwepo kwa vurugu na kwamba hali ya usalama inaendelea vizuri, akisema wananchi wanaendelea na shughuli zao.

“Waliojiorodhesha wengi wanadai wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao kwa kupigwa na fimbo na wengine wanadai wamepigwa na vitako vya bunduki,” alisema Mlokozi.

Mlokozi alisema pia walioharibiwa mali wengi wanadai wamepoteza fedha na simu na wengine kuharibiwa sehemu zao za biashara ambazo wanazitegemea kujipatia riziki.

“Hatujui kama watalipwa au la, tunasubiri majibu kwa DC baada ya kupokea haya majina na ripoti nzima ya tukio hili,” alisema.

Kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema tayari jeshi hilo limewakamata askari wawili na bado linaendelea na uchunguzi.

“Ni kweli tumekamata watu wawili ambao ni askari na bado tunaendelea na uchunguzi. Hivyo nitatoa ripoti kamili baada ya kukamilisha uchunguzi wetu,” alisema Mambosasa.

Wananchi hao wanadai kuwa askari wa kikosi cha FFU walikuwa wakienda kwenye mitaa ya eneo hilo na kumpiga kila waliyekutana naye na wengine kuingia majumbani wakiwa wameficha nyuso zao na kupora mali.

Wanadai kuwa kilichowafanya watambue kuwa ni askari ni suruali za sare walizokuwa wakivalia wakati wakiwa kwenye vurugu hizo, zilizohusisha pia kushusha watu waliokuwa katika usafiri wa pikipiki za matairi matatu na hata mabasi ya daladala.

No comments:

Post a Comment

Popular